
.jpg)
Meneja Miradi wa YWL, Veronika Masawe akizungumza na vyombo vya habari.
Na Eunice Kanumba.
Shirika la Young Women Leadership (YWL) limeendelea kutekeleza mradi wa “Mwanamke ni Sehemu ya Maamuzi, Shiriki Naye”, unaolenga kuwawezesha wanawake vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 kushiriki kikamilifu katika michakato ya maamuzi na maendeleo ya jamii.
Kupitia mradi huo, shirika hilo linaendelea na mchakato wa kuunda vikundi vya msaada na uwezeshaji kwa wanawake vijana katika kila kijiji kilichopo kwenye kata zinazotekeleza mradi ambazo ni Kizumbi na Mwawaza.
Hatua hiyo imeendelea kutekelezwa leo, Septemba 24, 2026, ambapo YWL imefanikiwa kuunda kikundi cha wanawake vijana katika kijiji cha Nhelegani, Kata ya Kizumbi, chenye jumla ya wanachama 30 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 35.
Akizungumza baada ya kutoa elimu na kuunda kikundi hicho, Meneja Miradi wa YWL, Veronika Masawe, amesema elimu iliyotolewa inalenga kuwajengea wanawake vijana uwezo wa kujiamini, kushiriki katika vikao vya maamuzi, kutunza afya zao pamoja na kujisimamia katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Masawe amesema mradi huo umefika kwa wakati muafaka, kwa kuwa utawasaidia wanawake vijana kujenga uwezo wa kupinga vitendo vya rushwa ya ngono, kutumia fursa zilizopo katika jamii na kushiriki katika vyombo mbalimbali vya maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi jamii kwa ujumla.
“Kama mnavyoona hapa, tayari tumeshaunda kikundi ambacho kina wajumbe 30, ambao ni wanawake vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35,” amesema Masawe.
Aidha, Masawe ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa wanawake vijana wanaounda vikundi hivyo katika kata za Kizumbi na Mwawaza, ikiwemo kuwajengea uwezo kisaikolojia na kuwaunga mkono katika masuala ya elimu, uchumi na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kizumbi, Livingstone Saria, amelishukuru shirika hilo kwa kutekeleza mradi huo katika kata hiyo, akisema umetoa elimu muhimu kwa wanawake vijana, hususan kuhusu uongozi na msaada wa kisaikolojia.
Saria amesema ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wanawake hao katika kutekeleza majukumu mbalimbali yanayohusiana na kikundi hicho, akieleza kuwa anaamini elimu waliyoipata itawasaidia kukabiliana na changamoto za kiuchumi kuanzia ngazi ya familia hadi jamii.
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi, Mwenyekiti aliyechaguliwa kuongoza kikundi hicho cha wanawake vijana katika kijiji cha Nhelegani, Mary Mathias, amesema elimu waliyoipata imewajengea uwezo na kuongeza kujiamini katika kushiriki masuala mbalimbali yanayohusu maisha na maendeleo yao.
Mary amesema kupitia kikundi hicho, wanatarajia kutumia elimu na fursa watakazozipata kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu familia na jamii yao.
.jpg)


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464