Wadau wa haki na amani wameshauri Tume ya Maridhiano inayotarajiwa kuundwa na serikali iwe shirikishi na itekeleze majukumu yake kwa kuzingatia ukweli ili kupata mwafaka wa kitaifa.
Rais Dk Samia Suluhu Hassan Julai 30 mwaka huu alisema kuwa serikali inakusudia kuunda tume hiyo ili kuharakisha mchakato wa marekebisho ya Katiba sambamba na kazi ya Tume ya Uchunguzi wa Jinai ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu 2025.
Akifafanua kuhusu mchakato huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben, alisisitiza kuwa ni muhimu tume hiyo iwe na uwakilishi wa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, vijana, wazee na walemavu na kuepuka mijadala ya mihemuko.
Naye Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura, amesema kuwa maridhiano ya kweli yanajengwa katika ukweli na kupendekeza kazi za tume zioneshwe kwa uwazi, zikijumuisha kulipwa fidia na kurejeshewa vitendea kazi kwa wanahabari waliopata madhila.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, akipendekeza tume hiyo ijumuishe vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya dola, na familia za waathirika ili kupitia kukiri makosa na uwajibikaji, taifa liweze kuponya majeraha yake.
Pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa NEC ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, wamesisitiza kuwa maridhiano ni njia sahihi na endelevu inayohusisha pia viongozi wa dini, asasi za kiraia na makundi yote ya Watanzania katika kudumisha amani na umoja wa nchi..
