` VIONGOZI WA DINI WATEMBELEA BANDARI WATAKA VIJANA KUKAMATA FURSA

WANDAMAN HOTEL

VIONGOZI WA DINI WATEMBELEA BANDARI WATAKA VIJANA KUKAMATA FURSA

 

Viongozi wa dini mkoani Mtwara wamewataka vijana kuongeza ujuzi na kusomea taaluma mbalimbali zitakazowawezesha kujiandaa na kuchangamkia fursa za ajira na biashara zinazotokana na uwekezaji unaofanyika katika Bandari ya Mtwara na Bandari ya Kisiwa Mgao.
Wamesema Bandari ya Mtwara imeendelea kufunguka na kuongeza shughuli za kiuchumi, hivyo vijana wanapaswa kujiandaa kitaaluma ili waweze kunufaika na fursa zinazojitokeza, ikiwemo ajira za udereva na taaluma nyingine.

Viongozi hao wamesema hayo wakati wa ziara ya viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali waliotembelea Bandari ya Mtwara pamoja na eneo la ujenzi wa Bandari ya Mizigo Michafu katika Kisiwa Mgao.

Wamesema kukamilika kwa Bandari ya Kisiwa Mgao kutasaidia kuongeza shughuli za usafirishaji wa mizigo michafu, ikiwemo saruji na makaa ya mawe, na hivyo kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi, hususani vijana.

Ziara hiyo imeandaliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mtwara, Asha Moto, kwa lengo la kuwawezesha viongozi hao wa dini kujionea uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali mkoani Mtwara pamoja na fursa za kiuchumi zinazofunguliwa kwa wananchi wa ukanda wa kusini.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464