TABORA: Diwani wa Kata ya Chemchem na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji, Ujenzi na Mazingira ya Manispaa ya Tabora, Bandora Salum Mirambo, amewaelekeza wenyeviti wa mitaa kushirikiana na Kamati za Maafa kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira na kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Bandora ametoa maelekezo hayo huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kufanya usafi katika maeneo yanayoweza kusababisha maji kutuama au kujaa, ikiwemo kusafisha mitaro na mifereji pamoja na kufukua misingi iliyoziba, ili kuhakikisha maji yanapata njia ya kupita na hivyo kupunguza hatari ya mafuriko.
Amesema wenyeviti wa mitaa wanapaswa kuchukua hatua za haraka katika maandalizi ya kukabiliana na majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatua za kujikinga na kupunguza madhara.
Bandora amesisitiza kuwa maandalizi hayo yanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Sura ya 242, inayoweka msisitizo katika hatua za kujiandaa, kuzuia na kupunguza athari za majanga.
Aidha, amewataka wenyeviti wa mitaa, kwa kushirikiana na kamati zao, kuimarisha ushirikiano na kuongeza uhamasishaji kwa wananchi ili wachukue tahadhari mapema kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwepo wa mvua za El Niño.
Amesema hatua za mapema za usafi na maandalizi zinaweza kusaidia kupunguza athari za mafuriko na kulinda maisha, mali pamoja na mazingira ya wananchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
