Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda cha Qatar (QCCI) kimeeleza kuwa Tanzania ni eneo muhimu sana la uwekezaji kutokana na mkao wake wa kijiografia na rasilimali ilizonazo.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu wa Kwanza wa QCCI, Mohammed Al Kuwari, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, pamoja na ujumbe wake jijini Doha, Qatar.
Al Kuwari alibainisha kuwa wafanyabiashara wengi wa Qatar wako tayari kuwekeza nchini Tanzania, lakini wanahitaji elimu zaidi na fursa ya kufahamiana na wafanyabiashara wenzao wa Kitanzania.
Alipendekeza kufanyika kwa warsha maalum na mikutano ya mtandaoni itakayozikutanisha sekta binafsi za nchi zote mbili ili kutoa elimu kuhusu fursa zilizopo, viwango vya ubora vinavyohitajika, na kuondoa vikwazo vya kibiashara, huku akisisitiza kuwa milango yao iko wazi kwa ajili ya ushirikiano.
Katika kikao hicho, pande zote mbili zilijadiliana masuala ya kiuchumi na uwekezaji, zikiainisha fursa zilizopo katika jumuiya za kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Baraza la Ushirikiano la Nchi za Kiarabu za Ghuba (GCC).
Aidha, kikao kiliafikiana kuhusu umuhimu wa kuzikutanisha taasisi za uwakilishi wa sekta binafsi zikiwemo Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), na QCCI ili kujadili kwa kina maeneo ya ushirikiano wa kimkakati wa kibiashara na uwekezaji.
Kwa upande wake, Dk. Mwigulu alisisitiza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi kwenye mipango ya maendeleo ya nchi, hasa kupitia Dira ya Maendeleo 2050 inayolenga kufikisha uchumi wa taifa thamani ya Dola za Marekani trilioni moja.