MAAFISA MAENDELEO SHY DC WAFANYA USAFI WA MAZINGIRA, WATOA MAHITAJI KWA WAZAZI TINDE
Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
Umoja wa Maafisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (SHY DC) umeadhimisha kilele cha Siku ya Maafisa Maendeleo kwa kufanya usafi wa mazingira na kutoa mahitaji muhimu kwa wazazi katika Kituo cha Afya Tinde, kilichopo Kata ya Tinde, ikiwa ni sehemu ya kurejesha fadhila kwa jamii.
TAZAMA VIDEO👇👇
Zoezi hilo limefanyika leo, Septemba 28, 2026, likishirikisha Umoja wa Maafisa Maendeleo pamoja na watumishi wa Kituo cha Afya Tinde, ambapo wamefanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho.
Zoezi hilo pia lililenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira, hususan kuelekea kipindi cha mvua kinachotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu, huku hatua hiyo ikitajwa kuwa sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.
Akizungumza kwa niaba ya mratibu wa zoezi hilo, Afisa Maendeleo Kata ya Usanda, Halima Tendega, amesema Umoja wa Maafisa Maendeleo unaendelea kutekeleza majukumu yake katika mazingira mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushiriki shughuli zinazolenga kuboresha ustawi wa jamii.
Amesema zoezi hilo ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kutunza mazingira na kuhakikisha maeneo wanayoishi na kupata huduma yanakuwa safi na salama.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Tinde, Dkt. Evance Munis, amepongeza Umoja wa Maafisa Maendeleo kwa hatua hiyo, akisema inakwenda sambamba na ajenda ya Serikali ya kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.
Dkt. Munis amesema kituo hicho kinaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi kwa ajili ya kulinda afya za watumishi pamoja na wananchi wanaofika kupata huduma.
Aidha, Dkt. Munis amepongeza utoaji wa mahitaji kwa wazazi na kuziomba taasisi mbalimbali kuendelea kushirikiana na kituo hicho, akieleza kuwa baadhi ya wazazi hufika kupata huduma za kujifungua wakiwa hawana mahitaji muhimu.



















