` MAHAFALI YA TATU YA SANTA EDWIN YAWA KIVUTIO

WANDAMAN HOTEL

MAHAFALI YA TATU YA SANTA EDWIN YAWA KIVUTIO

 


Na .Mwandishi wetu

Mwanza

Shule ya Santa Edwin Pre and Primary School, iliyopo Majengo Mapya, Nyegezi jijini Mwanza, imefanya Mahafali yake ya Tatu Septemba 24, 2026, huku ikijivunia mafanikio mbalimbali katika taaluma na malezi ya wanafunzi.

Mgeni Rasmi katika mahafali hayo alikuwa Barkat Firoz Khan, Afisa Rasilimali Watu kutoka Furaha Company Ltd ya jijini Mwanza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Khan aliipongeza shule hiyo kwa kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali, ikiwemo mitihani ya kitaifa, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.
“Nashauri walimu, watoto na wazazi kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha shule inatoa watoto wenye ufaulu mzuri na maadili mema,” alisema Khan.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Santa Edwin Lulu Samson Soko aliwahakikishia wazazi kuwa uongozi wa shule utaendelea kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora sambamba na malezi yenye misingi ya maadili mema.
Naye Hassan Ibrahimu, Mwalimu Mkuu wa Santa Edwin, alisema mafanikio ya shule hiyo yataendelea kujengwa kupitia umoja na mshikamano baina ya walimu, wazazi na uongozi wa shule.

Katika mahafali hayo, wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo na kuonesha umahiri katika maeneo mbalimbali walipewa zawadi, huku wafanyakazi wa shule nao wakitambuliwa na kutunukiwa zawadi kwa mchango wao katika kufanikisha maendeleo ya shule.
Santa Edwin Pre and Primary School inaendelea kujenga kizazi chenye elimu, uwezo na maadili mema kwa ajili ya Tanzania ya kesho.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464