Diwani wa Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Jackline Isaro, ameahidi kuendelea kushirikiana na wazazi katika kutatua changamoto zinazoikabili shule ya Sekondari ya Ngokolo, ikiwemo ukarabati wa madarasa na ujenzi wa uzio wa shule hiyo.
Akizungumza katika mahafali ya 18 ya Shule ya Sekondari Ngokolo, Mhe. Isaro amesema kuna uwezekano wa shule hiyo kupata madarasa mapya kutoka Serikalini ifikapo mwezi Desemba, huku akiwahimiza wananchi kutokuwa na hofu kuhusu hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto za miundombinu.
“Mwezi Desemba tunaweza kupata madarasa mapya kutoka kwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Niwatoe hofu kupitia risala hii. Naomba niseme madarasa hayo tutayakarabati,” amesema Isaro.
Aidha, Diwani huyo ameahidi kuchangia mifuko 15 ya saruji ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusaidia kuboresha mazingira ya shule.
Mhe. Isaro pia amesema ataendelea kushirikiana na wananchi katika kipindi cha miaka mitano ambacho wamempa dhamana ya kuwaongoza katika Kata ya Ngokolo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ngokolo, Mwl. James Msimba awali akisoma taarifa ya shule katika mahafali hayo, ameeleza baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo.
Miongoni mwa changamoto hizo ni uchakavu wa vyumba saba vya madarasa, upungufu wa matundu 22 ya vyoo kwa wanafunzi pamoja na kukosekana kwa uzio wa kudumu katika eneo la shule.
Mkuu huyo wa shule amewasihi wahitimu kujitambua, kuwa na nidhamu na kutumia elimu waliyopata kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.
Betha Deus wakati akisoma risala ya wahitimu katika mahafali hayo kuwa wanafunzi hao wamejiandaa kufanya vizuri katika mtihani wao wa kuhitimu na kwamba wataendelea kutumia nidhamu na elimu waliyopata kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla .
Jumla ya wahitimu 364 katika shule ya sekondari Ngokolo wamesherehekea siku yao ya kuhitimu kidato cha nne 2026. 













