Na Marco Maduhu, NZEGA
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, wamejadili masuala mbalimbali ya maendeleo katika kikao cha baraza, kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi na kuinua maendeleo ya wilaya hiyo.
Kikao hicho cha Baraza la Madiwani kimefanyika leo, Septemba 10, 2026, ikiwa ni kikao cha Robo ya Nne, kinachohusu kipindi cha Aprili hadi Juni 2026, kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Awali, madiwani hao walipowasilisha taarifa za Kata zao, pamoja na kuipongeza halmashauri kwa kazi inayofanya katika kuwahudumia wananchi, waliwasilisha pia kero zinazowakabili wananchi, ikiwamo ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, umeme na uchakavu wa miundombinu ya elimu.
Mmoja wa madiwani hao Kiabo Mbozu wa Kata ya Isanzu, amesema ubovu wa miundombinu ya barabara umekuwa changamoto kubwa kwa wananchi katika kufanya shughuli zao za kiuchumi.
“Ubovu wa miundombinu ya barabara umekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Kata ya Isanzu, hasa katika kufanya shughuli zao za kiuchumi. Hali hii inasababisha usafiri kuwa mgumu na kuathiri shughuli mbalimbali za wananchi, hivyo tunaomba changamoto hii ishughulikiwe ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.” Amesema Kiabo.
Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Nzega, Mhandisi Hans Makisa, akitoa majibu kwa madiwani hao, amesema baadhi ya barabara zipo katika hatua za utekelezaji, huku nyingine zikiwa tayari zimeingizwa kwenye mipango ya bajeti.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Aron Maganga, ameiagiza TARURA kuchukua kero zote zilizowasilishwa na madiwani na kuzifanyia kazi, pamoja na kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara ili ihakikishe inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Aron Maganga akizungumza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega Mwarami Seif.