Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,ameitaka Wizara ya Nishati kusimamia ukamilishaji wa haraka wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme kote nchini, ili umeme unaozalishwa katika Kituo cha Julius Nyerere ufike katika maeneo yenye mahitaji ya uzalishaji na uwekezaji.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo, tarehe 22 Agosti, 2026, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere, Rufiji, mkoani Pwani.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kunapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika uzalishaji, viwanda, biashara, madini, kilimo cha kisasa, huduma za kijamii, uwekezaji na ajira.
Kituo hicho, chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, kinachangia takribani nusu ya umeme unaoingizwa katika Gridi ya Taifa, hatua iliyoimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.
Ongezeko hilo, amesema Rais Dkt. Samia, limeimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuondoa changamoto zilizokuwa zikiathiri shughuli za uzalishaji, uchumi na huduma nyingine muhimu.
“Mradi huu umethibitisha uwezo wetu Watanzania. Tuutumie kusukuma miradi mingine ya kimkakati ili tuweze kujenga Taifa thabiti na linalojitegemea,” amesema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amesema kukamilika kwa kituo hicho ni matokeo ya fikra na maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, yaliyoendelezwa katika awamu mbalimbali za uongozi hadi sasa.
Katika hilo, ametambua mchango wa Marais waliomtangulia, hususan Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye, katika awamu yake ya uongozi, alichukua hatua thabiti za kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo muhimu kwa Taifa, mwaka 2019.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amewaasa Watanzania kulinda amani na utulivu wa nchi, sambamba na kuimarishwa kwa ulinzi wa miundombinu, mazingira na vyanzo vya maji vinavyotegemewa na kituo hicho ili kiendelee kufanya kazi kwa ufanisi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Dkt. Mostafa Madbouly, ameipongeza Tanzania kwa kukamilisha kituo hicho, akisema mafanikio hayo yamedhihirisha uwezo wa ushirikiano wa Afrika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
“Kukamilika kwa kituo hiki kunadhihirisha uwezo wa kampuni za Misri katika kutekeleza miradi mikubwa kwa kiwango cha kimataifa, hasa barani Afrika,” amesema Dkt. Madbouly.

Ameongeza kuwa, kukamilika kwake kunafungua nafasi ya kukuza ushirikiano zaidi kati ya Tanzania na Misri katika biashara, uwekezaji, ujenzi, barabara, bandari, kilimo, umeme na nishati.
Naye, Waziri wa Nishati, Mhe. Deo Ndejembi, amesema Serikali inaendelea kujenga njia kusafirisha umeme ya kilovolti 400 ya Iringa–Mbeya–Songwe–Rukwa, iliyofikia asilimia 98, pamoja na njia za Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika na Tanzania–Uganda ili kuunganisha vituo vya uzalishaji, maeneo ya shughuli za kiuchumi na masoko ya kikanda.
Ameongeza kuwa, Tanzania imeanza mazungumzo ya kuuza umeme nchini Zambia, pamoja na makubaliano ya kubadilishana umeme na nchi ya Kenya, na inaendelea na majadiliano hayo na nchi nyingine jirani.
Akiwasilisha salamu zake, Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina, amesema kituo hicho kinaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa nishati na shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Mmepata nguvu; sasa tumieni nguvu hiyo kujenga mustakabali,” amesema Dkt. Adesina, akieleza kuwa nishati ya uhakika itaongeza thamani ya rasilimali, biashara na ajira.
Ujenzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere ulianza mwaka 2019 kwa gharama ya shilingi trilioni 7.452. Kituo kina mitambo tisa yenye uwezo wa
kuzalisha jumla ya Megawati 2,115, jengo la mitambo, transfoma 27 na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwa msongo wa Kilovolti 400.







.jpeg)








