` MRADI WA UPANUZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM ENEO LA KURASINI WAFIKIA ASILIMIA 98

WANDAMAN HOTEL

MRADI WA UPANUZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM ENEO LA KURASINI WAFIKIA ASILIMIA 98



Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam katika eneo la zamani la EPZA Kurasini umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kuanza kutoa huduma rasmi baada ya miezi miwili.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo hilo la mradi, Waziri Mbarawa alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha bandari hiyo kuongeza uwezo wake wa kuhudumia makasha hadi 700,000 kwa mwaka kutoka uwezo wa sasa wa kuhudumia makasha 344,000 pekee, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa makasha na malori huku likiongeza ufanisi wa utoaji wa mizigo.

Mradi huo unaotekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 224,000 umegawanywa katika awamu mbili kuu, ambapo awamu ya kwanza yenye ukubwa wa mita za mraba 84,000 imefikia asilimia 98 ya utekelezaji na inatazamiwa kukamilika mwezi ujao ili iweze kuanza kuhudumia hadi makasha 150,000 kwa mwaka.

Awamu ya pili yenye ukubwa wa mita za mraba 140,000 imepangwa kukamilika mwezi Machi 2027 na itachangia kuongeza uwezo wa kituo hicho kwa makasha mengine 550,000 kwa mwaka, hatua inayotajwa na serikali kama suluhu ya kudumu ya kukabiliana na ongezeko kubwa la shughuli za kibandari.

Profesa Mbarawa alisisitiza kuwa wananchi na wadau mbalimbali wanaotumia bandari hiyo hawataki tena kusikia takwimu za utekelezaji bali wanataka kuona matokeo na manufaa ya mradi huo pindi utakapotoa huduma.

Alifafanua kuwa serikali imeamua kulitumia eneo hilo kama kituo maalum ambapo makasha yatakaposhushwa bandarini yatasafirishwa moja kwa moja hadi Kurasini kwa ajili ya shughuli za ukaguzi na uondoshaji wa mizigo kupitia vifaa vya kisasa kama mashine za skana kabla ya kuchukuliwa na wamiliki, mfumo ambao utaanza na mizigo inayoingia nchini kabla ya kufuatiwa na bidhaa zinazotoka nje.

Akizungumzia chanzo cha mradi huo, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus Abed, alieleza kuwa uamuzi huo umechochewa na ongezeko kubwa la ujazo wa mizigo iliyopita katika bandari hiyo jambo lililosababisha msongamano mkubwa wa makasha na malori, na hivyo kituo hicho kipya kitakapokamilika kitaondoa makasha katika eneo la uendeshaji mkuu wa bandari na kutoa nafasi ya kutosha kwa ajili ya shughuli za upakiaji na upakuaji wa meli.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464