` TAMASHA LA MICHEZO SHULE ZA SEKONDARI SHINYANGA KOMBE LA DC MTATIRO LAFANA

WANDAMAN HOTEL

TAMASHA LA MICHEZO SHULE ZA SEKONDARI SHINYANGA KOMBE LA DC MTATIRO LAFANA


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Tamasha la michezo lililowashirikisha wanafunzi na walimu kutoka shule mbalimbali za sekondari za Manispaa ya Shinyanga, maarufu kama Kombe la Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, limefana huku washindi wakizawadiwa zawadi mbalimbali.

TAZAMA VIDEO👇👇



Tamasha hilo lilifanyika leo Julai 29, 2026, katika viwanja vya shule ya Sekondari Old Shinyanga, likihusisha michezo mbalimbali ikiwamo kufukuza kuku, kukimbia na magunia, mbio za mita 100, kuvuta Kamba, kukimbia na mayai kwa kutumia vijiko, pamoja na fainali ya mpira wa miguu kati ya wanafunzi wa kidato cha nne na kidato cha sita wa shule ya Sekondari Old Shinyanga.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa tamasha hilo, Kaimu Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Manispaa ya Shinyanga Richard Makoye, amesema limewawezesha walimu na wanafunzi kukutana pamoja, kuimarisha afya, kujenga mahusiano na kuongeza ari ya kufanya kazi na kujifunza ili kuendelea kufanya vizuri kitaaluma.
"Kwanza kabisa tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa maelekezo na kuwezesha sekta ya elimu nchini, na Manispaa ya Shinyanga imeendelea kuwa miongoni mwa halmashauri zinazotekeleza kwa ufanisi sera za elimu, ikiwamo kushiriki matamasha ya michezo yenye lengo la kukuza taaluma," amesema Makoye.

Pia, amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, kwa kuanzisha na kuendelea kuunga mkono matamasha hayo ya michezo shuleni, ambayo yamekuwa chachu ya ukuzaji wa taaluma.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amesema aliahidi kuandaa Tamasha la michezo kwa walimu na wanafunzi, na sasa ahadi hiyo imetekelezwa kwa mafanikio makubwa.

Amesema tamasha hilo limeimarisha umoja na ushirikiano miongoni mwa walimu, limewapa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuongeza ari pamoja na mbinu za ufundishaji.
Aidha, amesema ataendelea kuhamasisha mabonanza ya michezo ndani ya shule, na kwamba hivi karibuni atazindua ligi ya mkuu wa wilaya itakayoshirikisha shule zote za sekondari.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndala Hamisa Magulu, amesema bonanza hilo limekuwa na manufaa makubwa kwa walimu na wanafunzi, kwa kuwa limeongeza ushirikiano kati ya shule mbalimbali, na kusaidia kupunguza changamoto za afya ya akili.
Mmoja wa wanafunzi Daud Charles wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga, amesema michezo hiyo imewasaidia kujenga afya, kuimarisha ushirikiano, na kuongeza morali ya kufanya vizuri katika masomo.

VIDEO👇

Katika tamasha hilo, washindi mbalimbali walikabidhiwa zawadi, huku walimu na shule zilizofanya vizuri kitaaluma zikitunukiwa vyeti vya pongezi. Aidha, washindi wa fainali ya mpira wa miguu kwa upande wa kidato cha sita kutoka Shule ya Sekondari Old Shinyanga walikabidhiwa kombe, mbuzi watatu na vinywaji, baada ya kuiwafunga kidato cha Nne magoli mawili kwa bila.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akikabidhi Kombe kwa Timu ya Kidato cha Sita shule ya Sekondari Oldshinyanga baada ya kuibuka washindi katika Tamasha la Michezo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akichezesha fainali.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464