` BARAZA LA MADIWANI SHINYANGA LAIBUA CHANGAMOTO ZA MAJI, UMEME NA MIUNDOMBINU SHULENI

WANDAMAN HOTEL

BARAZA LA MADIWANI SHINYANGA LAIBUA CHANGAMOTO ZA MAJI, UMEME NA MIUNDOMBINU SHULENI



Na Suzy Butondo, Shinyanga 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga limeibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hususan ukosefu wa maji, umeme na miundombinu muhimu katika baadhi ya shule na vijiji, huku likitaka wataalamu na wakuu wa idara kuzifanyia kazi changamoto hizo.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani cha kuwasilisha taarifa za kata, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga, Seth Anthony Msangwa, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Madiwani wameeleza kuwa baadhi ya shule, zikiwemo Shule ya Msingi Mwambasha na Mwasingu, zinakabiliwa na ukosefu wa maji, hali ambayo inaathiri mazingira ya kujifunzia na usafi wa wanafunzi, pia wameomba kuboreshwa kwa vyoo vya kisasa katika shule hizo.

Aidha, imeelezwa kuwa Shule ya Msingi Mwabenda inahitaji vyoo ili kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia.

Diwani wa Kata ya Usule, Masanja Seni Ngasa, amesema Shule ya Igalamya imejengwa eneo la mlimani na licha ya jitihada za kuchimba maji, bado changamoto hiyo haijapatiwa ufumbuzi. 

Amesema ukosefu wa maji na umeme umekuwa sababu ya baadhi ya walimu kukimbia kituo hicho cha kazi, kwa mujibu wa diwani huyo, walimu na wananchi hulazimika kutembea umbali wa takribani kilomita sita kutafuta maji, hali inayowalazimu kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo badala ya kuzingatia shughuli za elimu na uzalishaji.

Amesema changamoto hiyo pia inaweza kuwa na athari kwa wanafunzi, wakiwemo watoto wa kike, kutokana na mazingira magumu wanayokutana nayo shuleni na majumbani.

Kwa upande wake, diwani wa Kata ya Iselamagazi, Isack, amesema pamoja na baadhi ya vijiji kuwa na huduma ya maji, bado kuna vitongoji vinavyokabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, akitolea mfano Kitongoji cha Mpembo Mwabundala na Kitongoji cha Nhendegese.

Ameiomba RUWASA kuongeza nguvu katika maeneo hayo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika.

Chalya Bugeta ambaye ni diwani wa kata ya Lyabusalu ameeleza changamoto za barabara, maji na umeme katika maeneo mbalimbali, Mwasingu na Mwambasha, huku akisisitiza kuwa huduma hizo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wananchi.

AidhaMwenyekiti Msangwa amewaomba wataalamu na wakuu wa idara kuhakikisha hoja zote zilizotolewa na madiwani zinafanyiwa kazi kwa uadilifu ili viongozi wanaporudi kwa wananchi waweze kutoa majibu yenye ukweli na utekelezaji wa vitendo.

“Changamoto zote zilizotajwa hapa zikafanyiwe kazi ili tukirudi kwa wananchi tusiwadanganye,” amesema Msangwa, huku akiwataka wataalamu na wakuu wa idara kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Amesema Halmashauri ina watumishi, wadau na wananchi walio tayari kushiriki katika kutatua changamoto za maendeleo, hivyo ni muhimu nguvu hizo zikaunganishwa, pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha shule zote zinazokabiliwa na changamoto ya maji zinapatiwa huduma hiyo, ikiwemo kuchimbwa visima pale inapohitajika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Edward Ngelela amewapongeza madiwani kwa kufanya vizuri katika kuibua na kusimamia hoja za wananchi, akitaka hoja hizo zifanyiwe kazi na wataalamu ili ziwe na majibu yanayoonekana kwa wananchi.

Aidha, katibu tawala wa wilaya hiyo  Said Kitinga amesema ni muhimu kuzingatia mahitaji ya kina mama wajawazito na watoto, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana katika kuupokea Mwenge wa Uhuru, ambao unatarajiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kushirikiana kwa pamoja katika kuupokea Mwenge wa Uhuru na kutumia fursa hiyo kuonyesha miradi inayotekelezwa kwa manufaa ya jamii.

Viongozi hao wamewataka wananchi kuendelea kupendana na kushirikiana katika shughuli za maendeleo, wakisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni msingi wa kupiga hatua katika kuboresha huduma za kijamii kama maji, elimu, umeme na barabara.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga Seth Anthony Msangwa akizungumza kwenye kikao
Mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga akizungumza
Madiwani wa halmashauri ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha baraza






































 

 





 








 



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464