` FITCH YATOA B CHANYA, YATANGAZA UCHUMI WA TANZANIA KUENDELEA KUIMARIKA

WANDAMAN HOTEL

FITCH YATOA B CHANYA, YATANGAZA UCHUMI WA TANZANIA KUENDELEA KUIMARIKA



Kampuni ya kimataifa ya Fitch Rating inayojihusisha kufanya tathmini ya uwezo wa nchi kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa imetoa alama ya B chaya hatua inayodhihirisha kuimarika kwa misingi ya uchumi na uimara wa sera za uchumi jumla nchini.

Ripoti ya tathmini ya kampuni hiyo iliyochapishwa katika tovuti rasmi, Fitch imesema mabadiliko hayo yanatokana na kuimarika kwa akiba ya fedha za kigeni, kuwepo kwa nakisi ya bajeti inayodhibitika na kuendelea kwa ukuaji wa uchumi, mambo ambayo kwa pamoja yanatarajiwa kuongeza mapato kusaidia kuhudumia bajeti ya nchi pamoja na kupunguza mzigo wa deni la serikali.

Aidha, Fitch imesema akiba ya fedha za kigeni nchini inatarajiwa kuongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 6.3 mwishoni mwa mwaka 2025 hadi kufikia Dola bilioni 7.9 mwaka 2028, sawa na uwezo wa kugharimia malipo ya nje kwa takribani miezi 3.3.

Fitch imeeleza kuwa kupungua kwa changamoto katika soko la fedha za kigeni na kuongezeka kwa unyumbufu wa kiwango cha ubadilishaji wa fedha kumechangia kupunguza baadhi ya hatari za muda mfupi, huku akiba ya dhahabu isiyo ya fedha inayomilikiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 2.4, inaweza kuongeza zaidi kinga ya nchi dhidi ya mishituko ya nje.

Katika upande wa bajeti na usimamizi wa deni, Fitch imekadiria kuwa nakisi ya bajeti kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2026 ilikuwa asilimia 2.8 ya Pato la Taifa ikichangiwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato na athari ndogo za ruzuku za mafuta katika utekelezaji wa bajeti.

Inatarajiwa nakisi hiyo kubaki karibu asilimia tatu ya Pato la Taifa hadi mwaka wa fedha 2028, likizingatia kuendelea kwa uboreshaji katika ukusanyaji wa mapato kupitia Mpango wa Muda wa Kati wa Mapato.

Kampuni hiyo imebainisha kuwa mapato ya kodi yaliongezeka kutoka asilimia 14.6 hadi asilimia 15.6 ya pato la taifa kati ya mwaka wa fedha 2023 na 2025, huku ikitabiri kuwa deni la serikali kwa uwiano na pato la taifa litapungua kutoka asilimia 48.9 mwaka 2025 hadi asilimia 46.2 mwaka 2028, kiwango ambacho kitakuwa chini ya wastani wa asilimia 55 unaokadiriwa kwa nchi zilizo katika kundi la ukadiriaji wa B.

Imeeleza kuwa kupungua kwa deni kutachangiwa na ukuaji mkubwa wa pato la taifa kwa thamani ya sasa pamoja na nakisi ndogo ya msingi ya bajeti, wakati katika upande mwingine, Fitch imepongeza hatua zinazochukuliwa kuboresha usimamizi wa fedha za umma ikibainisha kuwa hadi Machi 2026, kiasi cha madeni yaliyothibitishwa ya serikali kwa wazabuni na marejesho ya kodi kilikuwa kimepungua hadi asilimia 0.2 ya pato la taifa kutoka asilimia 1.2 Desemba 2022.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi, kampuni hiyo ya kimataifa inatarajia Tanzania kuendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na wastani wa nchi zilizo katika kundi la B, ikitabiri ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 5.8 mwaka 2026 dhidi ya wastani wa asilimia 3.7 kwa kundi hilo na uchumi unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 6.1 katika kipindi cha 2027 hadi 2028, ukichochewa na uwekezaji wa umma, utalii, nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji na biashara kikanda pamoja na ukuaji wa sekta ya madini.

Wakati huo huo, Fitch inatarajia mfumuko wa bei wa wastani wa asilimia 4.2 mwaka 2026, kutoka asilimia 3.3 mwaka 2025 lakini ukiwa chini ya wastani wa asilimia 5.6 unaotarajiwa kwa nchi za kundi la B, huku ikieleza pia kuwa Tanzania imepiga hatua katika kuboresha mfumo wa sera za uchumi jumla tangu mwaka 2023 kupitia uboreshaji wa kitaasisi na kiutendaji ulioimarisha uhuru wa benki kuu, mfumo wa uendeshaji wa kiwango cha ubadilishaji wa fedha na usimamizi wa soko la fedha za kigeni.

Aidha, imeeleza kuwa uboreshaji huo unaweza kuongeza uwezo wa Tanzania kukabiliana na mishtuko ya kiuchumi, ingawa baadhi yake yanahitaji kuthibitishwa kupitia utekelezaji wake kwa muda, ambapo Fitch imehitimisha kwa kuona mwenendo wa uchumi wa Tanzania ukiwa na msingi chanya huku ikiweka mkazo katika kuendelezwa kwa nidhamu ya fedha, kuimarishwa kwa mapato ya ndani na utekelezaji endelevu wa uboreshaji wa sera ili kujenga mazingira imara zaidi ya uchumi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464