Serikali imesema Bandari ya Dar es Salaam imevunja rekodi ya kiwango cha kuhudumia makasha.Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema mwezi uliopita bandari hiyo ilihudumia makasha 138,000 ikilinganishwa na makasha kati ya 50,000 na 60,000 yaliyokuwa yakihudumiwa kwa mwezi mwaka 2021.
Msigwa alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kambi ya wapigania Uhuru Mazimbu mkoani Morogoro jana mchana.
Alisema katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 serikali iliweka lengo la bandari hiyo ihudumie mizigo tani milioni 28 lakini ilivuka lengo na kuhudumia tani milioni 39.8.
Msigwa alisema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji wa Sh trilioni tatu katika Bandari ya Dar es Salaam ili ihudumie mizigo mingi iwezekanavyo.
“Tangu mwaka 2021 serikali ilipofanya uamuzi wa kuipangisha Bandari ya Dar es Salaam kwa DP World, bandari yetu imepiga hatua kubwa sana, tuna gati 12 zinafanya kazi na zinajengwa gati nyingine 16 na hivi ninavyozungumza kati ya gati hizo tatu zinaendelea na ujenzi,” alisema.
Msigwa alisema ufanisi umeongezeka katika bandari hiyo na akabainisha awali meli zilikuwa zikisubiri hadi siku 46 lakini sasa mizigo inapita moja kwa moja, meli za mizigo zinashusha na kuondoka.
Pia, alisema serikali imeweka mkakati wa kuunganisha mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam na Reli ya Kisasa (SGR) ili mizigo hiyo isafirishwe kupelekwa Morogoro, Dodoma na vituo vingine vya mizigo.
Msigwa alisema serikali iliwekeza katika reli hiyo ili kila mtu aweze kushusha mzigo wake katika vituo hivyo na ikaendelea kwenye safari ya kwenda ambako anataka kwenda.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464