Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema serikali imeanza maandalizi ya kujenga Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika Kongwa mkoani Dodoma.Aidha amesema tayari serikali imetoa Sh bilioni moja kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu ili kuanza ujenzi wa kituo hicho.
Msigwa alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kambi ya wapigania Uhuru Mazimbu mkoani Morogoro Msigwa alisema ujenzi unaweza kuanza mwakani kwa sababu eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yaliyotunza historia kubwa ya Tanzania na mchango wake katika harakati za ukombozi wa nchi za Afrika.
Alisema maandalizi yameanza na michoro ya awali imeanza kupatikana huku serikali ikiwa imetenga fedha katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi huo.
“Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo na maandalizi yameanza. Tumeshapata michoro ya awali ya kujenga kituo cha urithi wa ukombozi wa Afrika Kongwa,” alisema Msigwa.
Alisema kituo hicho kinatarajiwa kuwa chuo kikubwa cha kisasa chenye hadhi ya kuwa kituo cha Afrika cha urithi wa historia ya ukombozi wa Afrika.
Alisema eneo la Mazimbu lina historia kubwa ya harakati za ukombozi wa Afrika Kusini ambako wapigania uhuru kutoka nchi hiyo waliishi na kujiandaa kwa mapambano ya ukombozi.
Msigwa alisema baadhi ya wapigania uhuru waliopoteza maisha walifanyiwa ibada na baadaye kuzikwa katika eneo hilo na takribani watu 97 wenye asili ya Afrika Kusini wakiwa wamezikwa Mazimbu.
Alisema serikali imefanya sensa na kubaini kuwapo takribani watoto 92 wa ndugu za wapigania uhuru wa Afrika Kusini waliowahi kupewa hifadhi Tanzania kwa ajili ya mapambano ya ukombozi wa Afrika Kusini.
Msigwa alisema eneo hilo limeendelea kutunzwa kama alama ya ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Alisema baadhi ya ndugu wa watu waliozikwa hapo wamekuwa wakifika Morogoro kwa ajili ya kuwatembelea ndugu zao.