
📌 Naibu Katibu Mkuu afungua rasmi kikao kazi kwa wadau
📌 Asema Sekta ya Utalii, Wanyanyamapori na Malikale ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa Taifa
📌 Kutoa vipaumbele vinavyopimika kufikia lengo la watalii milioni 8 ifikapo 2030
Na Neema Chalila Mbuja
NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nkoba Mabula leo Julai 27, 2026 amefungua rasmi Kikao Kazi cha Wadau wa Sekta ya Utalii kujadili Rasimu ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2030, wenye lengo la kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa pamoja wa malengo yaliyowekwa na vipaumbele vyake.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichojumuisha wadau wa Sekta ya Utalii wakiwemo Wakurugenzi wa Idara za Wanyamapori, Utalii na Malikale, Bw. Mabula amesema mchango wa wadau wa sekta hiyo ni muhimu kwani wao ndio watekelezaji wa mipango, mikakati na vipaumbele mbalimbali vilivyowekwa na Wizara na ndio maana wamealikwa ili kutoa maoni yao juu ya Mpango Mkakati huo ili kufikia malengo yaliyowekwa.
“Kuelekea lengo la kufikia watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030 niwaombe wadau kushirikiana na Wizara ili kuhakikisha malengo yanafikiwa na kuongeza pato la Taifa,” amesema Bw. Mabula.
Akiwasilisha Rasimu ya Mpango Mkakati huo wa Wizara, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Abdullah Mvungi amesema Rasimu ya Mpango Mkakati huo wa Wizara imeainisha ni nini Wizara inataka kufanya, ni vipaumbele gani vya utekelezaji na ni malengo yapi yanapimika sambamba na viashiria vya utekelezaji ili kufikia malengo mahususi.
Amesema Rasimu ya Mpango Mkakati wa Wizara imeandaliwa kwa kuangalia vipaumbele vya utekelezaji kwa upande wa Serikali ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa na Ukimwi, uelekeo wa Dira 2050 ambayo inaitaka Wizara kuhakikisha idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii vinaongezeka, sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025.
Kwa upande wa wadau waliotoa maoni ya utekelezaji wa Mpango Mkakati huo wameipongeza wizara kwa kuandaa rasimu iliyogusa maeneo yote ya utekelezaji na kuahidi kushirikiana bega kwa bega na Wizara ili malengo mahususi hayo yaweze kufikiwa.
Miongoni kwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na kuongeza nguvu ya kutangaza vivutio vya utalii, kutunza urithi wa malikale na kushirikisha zaidi jamii kwenye shughuli za uhifadhi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464















