BILIONI 204.4 KUTEKELEZA AWAMU YA PILI YA MRADI WA UMEME WA JUA KISHAPU
Na Marco Maduhu, KISHAPU
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi, amesema Serikali itatumia sh. bilioni 204.4 kutekeleza awamu ya pili ya Mradi wa Umeme wa Jua katika Kijiji cha Ngunga, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, utakaozalisha megawati 100 za umeme na kuziingiza kwenye Gridi ya Taifa.
TAZAMA VIDEO👇👇
Ndejembi alisema hayo leo Julai 27, 2026, wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kati ya Serikali na mkandarasi, iliyofanyika katika eneo la mradi, Kijiji cha Ngunga.
Amesema awamu ya kwanza ya mradi huo, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50, imekamilika na umeme wake tayari umeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Alisema utekelezaji wa awamu ya pili utaongeza megawati 100, hivyo kufanya jumla ya uzalishaji kufikia megawati 150.
"Sekta ya nishati ni muhimili wa maendeleo. Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana katika viwanda, migodi, afya au elimu bila kuwepo kwa umeme wa uhakika," amesema Ndejembi.
Aidha, amemwagiza mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya miezi 17 kwa kuzingatia masharti yote ya mkataba, ikiwamo viwango vya ubora, usalama mahali pa kazi na ulinzi wa mazingira.
Pia ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka mradi huo ili washiriki kuilinda miundombinu yake, pamoja na kuhakikisha mkandarasi anatoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wa maeneo husika.
Mbali na hayo, Waziri Ndejembi aliagiza kujengwa kwa madarasa matano kupitia utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alisema kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo kumeongeza megawati 50 kwenye Gridi ya Taifa na kuongeza vyanzo vya uzalishaji wa umeme nchini.
Amesema umeme wa jua ni chanzo cha nishati chenye gharama nafuu na rafiki kwa mazingira, huku ukichangia utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030.
Twange alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitia saini, Desemba 6, 2024, mkataba wa mkopo nafuu na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wenye thamani ya euro milioni 75.9 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa umeme wa jua wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100.
TAZAMA PICHA👇👇
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi akizungumza.
Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba akizungumza.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba akizungumza.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange akiwasilisha taarifa ya mradi.
Mbunge wa Kishapu Lucy Mayenga akizungumza.
Mfadhiri wa Mradi kutoka AFD akizungumza
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO Zuhura Bundala akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi akishuhudia utiaji saini mradi wa umeme Jua awamu ya Pili Megawati 100 unaotekelezwa katika kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu baina ya Mkandarasi na Serikali.
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi akishuhudia utiaji saini mradi wa umeme Jua awamu ya Pili Megawati 100 unaotekelezwa katika kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu baina ya Mkandarasi na Serikali.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464






