` WANAWAKE WAASWA KUWA MSTARI WA MBELE KATIKA KULINDA AMANI NA KULEA WATOTO KWA MAADILI

WANDAMAN HOTEL

WANAWAKE WAASWA KUWA MSTARI WA MBELE KATIKA KULINDA AMANI NA KULEA WATOTO KWA MAADILI


Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Rehema Nhamanilo,akizungumza
Suzy Butondo, Shinyanga

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Rehema Nhamanilo, amewataka wanawake kuendelea kuwahimiza vijana kulinda amani ya nchi pamoja na kuwafundisha watoto maadili mema ya Kitanzania.

Nhamanilo amesema hayo leo alipokuwa akizungumza na wanawake wa kata za Kolandoto, Ibadakuli na Chanaguha katika ziara ya kuwashukuru kwa ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa Rais, wabunge na madiwani. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda amani na kuepuka kupotoshwa na baadhi ya watu wenye nia ya kuvuruga utulivu wa nchi.

"Kuna vijana na watoto wetu wanaojiingiza katika makundi yenye mienendo isiyofaa ambayo hupotosha jamii na kusababisha uvunjifu wa amani. Ni wajibu wetu kuwashauri waachane na makundi hayo na badala yake washiriki katika kulinda amani ya Tanzania na kujiepusha na vitendo vya vurugu," amesema Nhamanilo.

Ameongeza kuwa wazazi wanapaswa kuwahimiza watoto wao kuepuka kushiriki katika maandamano au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, huku akiwataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuliongoza kwa amani na utulivu.

"Tuwasihi watoto wetu wasijihusishe na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi. Pia tuendelee kuliombea Taifa letu na Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kuliongoza kwa hekima na amani," amesema.

Aidha, amewashauri wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao ili kuwajenga katika maadili mema, huku akiwataka kuacha matumizi ya adhabu kali zinazoweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo vifo, akieleza kuwa vitendo hivyo ni ukatili dhidi ya watoto.

"Wazazi wenzangu, tupunguze hasira kwa watoto wetu na tuepuke kuwadhalilisha kwa kuwaita majina yasiyofaa. Tuwaite kwa majina yao na tuwalee kwa upendo ili wajenge tabia njema," ameongeza.

Akizungumzia masuala ya kiuchumi, Nhamanilo amewahimiza wanawake kujiunga na vikundi vya mikopo isiyo na riba na kuepuka mikopo yenye masharti magumu ambayo mara nyingi husababisha migogoro katika familia. Pia amewashauri kubuni na kuendeleza miradi ya kuongeza kipato, ikiwemo kilimo cha bustani na ufugaji.

Vilevile, amewataka wanachama kuendelea kulipa ada zao kwa wakati na kuwahamasisha wananchi wengine kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akibainisha kuwa bado kuna watu wengi wanaopiga simu wakihitaji kusajiliwa kuwa wanachama.

Kwa upande wao, baadhi ya wanawake walieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuiomba Kamati ya Utekelezaji kuzifikisha kero hizo kwenye mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi



o



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464