Wananchi wa Kata ya Mbuyuni, Wilaya na Mkoa wa Songwe, wametakiwa kujihepusha na matukio ya mauaji katika jamii na kutakiwa kuachana na tabia zinazochochea vitendo hivyo ili kuendelea kudumisha amani, usalama na utulivu katika maeneo yao.
Wananchi wa Kata ya Mbuyuni, Wilaya na Mkoa wa Songwe, wametakiwa kujiepusha kabisa na matukio ya mauaji katika jamii na kuachana na tabia zinazochochea vitendo hivyo ili kuendelea kudumisha amani, usalama na utulivu katika maeneo yao.
Hayo yalisemwa Julai 22, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi wa kata hiyo kupitia kampeni ya Serikali Nyumbani Kwako, inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu.
Kamanda Senga alieleza kuwa matukio mengi ya mauaji yanayotokea katika jamii husababishwa na migogoro ya kifamilia, wivu wa kimapenzi, imani potofu za kishirikina pamoja na wananchi kujichukulia sheria mkononi badala ya kufuata taratibu za kisheria, huku akiwataka wananchi hao kuachana na tabia hizo na kutumia njia za mazungumzo pamoja na vyombo husika kutatua migogoro ili kulinda usalama wa jamii.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Polisi Kata na viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mapema kabla ya madhara kutokea.
Aidha Kamanda Senga alisisitiza kuwa ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi na kwamba hakuna mtu anayepaswa kujichukulia sheria mkononi, akiongeza kuwa jamii yenye mshikamano na ushirikiano ndiyo msingi mkuu wa kudumisha amani na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.



