
Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Shinyanga mjini Rehema Nhamanilo akizungumza na wanawake wa kata ya Old Shinyanga, Mwamalili na Chibe
Suzy Butondo, Shinyanga
Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini umeendelea na ziara ya kukutana na wanachama wake kuanzia ngazi ya kata hadi shina, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha umoja, uhai wa chama na kusikiliza changamoto zinazowakabili wanachama.
Leo, Julai 23, 2026, Kamati ya Utekelezaji ya UWT Wilaya, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Rehema Nhamanilo, ilitembelea kata za Mwamalili, Old Shinyanga na Chibe, ambako ilifanya vikao vya ndani na wanachama wa jumuiya hiyo pamoja na kupokea maoni, ushauri na kero mbalimbali.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Nhamanilo aliwahimiza wanachama kuhakikisha wanalipa ada za UWT na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wakati, akieleza kuwa ada ni nguzo muhimu katika kuimarisha uhai wa chama na kusaidia utekelezaji wa shughuli zake.
Katika maeneo yote yaliyotembelewa, mwenyekiti huyo alipokea kero mbalimbali kutoka kwa wanawake, Kero hizo zilijibiwa na wataalamu kutoka idara mbalimbali waliokuwa wameambatana na Kamati ya Utekelezaji, ambao walitoa ufafanuzi na maelekezo kuhusu masuala yaliyowasilishwa.
Baadhi ya changamoto zilizoibuliwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara, huduma zisizoridhisha katika baadhi ya hospitali na vituo vya afya, pamoja na ombi la kutolewa kwa msamaha wa bima ya afya kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea.
Ziara hiyo inatarajiwa kuendelea kesho, Julai 24, 2026, ambapo Kamati ya Utekelezaji itatembelea kata za Mwawaza, Masekelo na Ibinzamata kwa lengo la kuendelea kuimarisha mawasiliano na wanachama pamoja na kusikiliza changamoto zao.
Katika ziara hiyo, Nhamanilo ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Wilaya pamoja na baadhi ya madiwani wa viti maalum, ambao wamekuwa wakishiriki katika kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowasilishwa na wananchi.
Ziara ya kata kwa kata ni sehemu ya mkakati wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini wa kuimarisha mshikamano wa wanachama, kuongeza ushiriki wao katika shughuli za chama, na kuhakikisha sauti za wanawake zinafika kwa viongozi kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464