Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano limezinduliwa rasmi leo, Julai 24, 2026, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga, na Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange, likiwa na lengo la kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni wa Wasukuma kupitia ngoma za asili, maonesho ya biashara, michezo ya watoto na shughuli mbalimbali za kijamii.
TAZAMA VIDEO👇👇
Tamasha hilo, ambalo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 24 hadi 26, 2026, linawakutanisha wadau wa utamaduni kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya Tanzania, huku likitoa fursa ya wananchi kujifunza mila na desturi za Wasukuma pamoja na kukuza biashara kupitia maonesho mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo, Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange, amesema tamasha hilo ni kielelezo cha umoja, mshikamano na amani ambayo Tanzania imeendelea kuienzi kwa miaka mingi.
Amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo na ndiyo inayowapa wananchi nafasi ya kusherehekea utamaduni wao, kutambua walikotoka, walipo na mwelekeo wa maisha yao.
"Nawashukuru wananchi wote kwa kufika kwenye tamasha hili la Utamaduni wa Msukuma. Nawaomba muendelee kujitokeza kwa wingi ili kwa pamoja tusherehekee, tuhifadhi na kuenzi utamaduni wetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," amesema Chifu Kidola wa Pili.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Shinyanga, Innocent Mtafi, amesema tamasha hilo lina mchango mkubwa katika kulinda na kuenzi utamaduni wa Mtanzania, huku likitoa fursa kwa vijana kujifunza mila na desturi za jamii zao.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha shughuli za utamaduni zinaendelea kupewa kipaumbele kwa kuwa ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Taifa na urithi wa vizazi vijavyo.
Naye mdau wa utamaduni kutoka Nairobi nchini Kenya, Dominic Mkami, wa kabila la Wakamba, amesema amesafiri hadi Shinyanga kushiriki tamasha hilo kwa lengo la kumuunga mkono mwandaaji wake, Peter Frank Lugumi (maarufu Mr. Black), kwa juhudi anazofanya katika kuhifadhi, kuendeleza na kuitangaza tamaduni ya Wasukuma.
Mkami amesema tamasha hilo limekuwa daraja muhimu la kuunganisha jamii mbalimbali za Afrika Mashariki kupitia utamaduni, huku likitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kijamii na kiuchumi.
Mratibu wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma, Peter Frank Lugumi (Mr. Black), ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo, akisema mbali na burudani za ngoma za asili, wageni watapata fursa ya kujifunza utamaduni wa Wasukuma, kutembelea mabanda ya biashara na kushiriki shughuli mbalimbali zitakazoendelea hadi Julai 26, 2026.
TAZAMA PICHA NA ELIZABETH COSMAS 👇👇
Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili Charles Njange akizungumza.
Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili Charles Njange akizungumza.
Msaidizi wa Chifu wa Kizumbi na Mratibu wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma Peter Frank Lugumi, Mr, Black akizungumza.
Naye mdau wa utamaduni kutoka Nairobi nchini Kenya, Dominic Mkami wa kabila la Wakamba, akizungumza.
















































































































