Mwenyekiti mpya wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Shinyanga, Hatibu Madata Mgeja
Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) Mkoa wa Shinyanga kimefanya uchaguzi wa viongozi wapya, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uongozi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kibinadamu kwa wananchi katika mkoa huo.
Uchaguzi huo umefanyika leo Julai 22,2026 amabao umelenga kupata viongozi watakaosimamia utekelezaji wa majukumu ya Chama cha Msalaba Mwekundu kwa ufanisi, pamoja na kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuwa kiungo muhimu katika kusaidia jamii, hususan wakati wa majanga na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti mpya wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Shinyanga, Madata Mgeja, amesema uongozi mpya umejipanga kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali pamoja na Serikali katika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wanaozihitaji.
Mgeja amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza nguvu katika utekelezaji wa shughuli za kibinadamu, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania Red Cross, Serikali na wadau wengine kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema uongozi mpya utazingatia kwa karibu mahitaji ya jamii na kuhakikisha kuwa Chama cha Msalaba Mwekundu kinaendelea kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi, ikiwemo kushiriki katika shughuli za kukabiliana na majanga na kutoa msaada kwa makundi mbalimbali yenye uhitaji.

Kwa upande wake, Meneja wa Kukabiliana na Maafa ambaye pia alikuwa Mjumbe Msaidizi wa Kamati ya Uchaguzi, Samwel Katamba, amesema uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa taratibu za chama na hufanyika kila baada ya miaka mitano, hatua inayowezesha wanachama kupata viongozi wapya wa kuendesha shughuli za chama.
Katamba amesema mchakato wa uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, huku akieleza kuwa viongozi waliochaguliwa sasa wana jukumu la kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi na malengo ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki katika mkutano huo wameeleza matarajio yao kwa uongozi mpya, wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano, kuongeza ubunifu na kuhakikisha huduma za Tanzania Red Cross zinawafikia wananchi wengi zaidi, huku wakitarajia uongozi huo kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha zaidi shughuli za kibinadamu katika Mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti mpya wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Shinyanga, Hatibu Madata Mgeja
