Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MSAIDIZI wa Chifu wa Utemi wa Kizumbi, ambaye pia ni mwandaaji wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma mkoani Shinyanga, Peter Frank Lugumi (maarufu kama Mr Black), amesema kuwa kuelekea msimu wa tano wa tamasha hilo, wamefanya matembezi ya amani kwa kutumia baiskeli wakishirikiana na wanafunzi.
TAZAMA VIDEO👇👇
Lugumi akizungumza katika matembezi hayo leo Julai 22,2026, amebainisha kuwa tamasha hilo la utamaduni (Sukuma Festival), ambalo litaenda sambamba na maonyesho ya biashara, litafanyika kuanzia Julai 24 hadi 26, 2026, katika viwanja vya shule ya msingi Nhelehani, Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.
Amesema, lengo la matembezi hayo ya baiskeli, ni kuwafundisha wanafunzi utamaduni wa kisukuma, ikiwa ni pamoja na kufahamu umuhimu wa baiskeli kama chombo kikuu cha usafiri, kilichobeba alama ya umoja na ushirikiano katika shida na raha tangu zama za kale.
“tunawafundisha vijana hawa, wasisahau utamaduni wao, na leo tumetembea nao kwa ajili ya hamasa, kuelimisha jamii na wao kuwavika uhusika wa utamaduni, na zaidi kufikisha ujumbe wa kulinda amani ya nchi yetu,” amesema Lugumi.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Shinyanga Innocent Matafi, amesema tamasha hilo linawapa nguvu kubwa ya kuendelea kushirikiana na jamii.
Amesisitiza kuwa, utamaduni unapaswa kuhifadhiwa vizuri, ambapo una faida kubwa katika kutunza historia, kutoa malezi bora, na kuwalea watoto katika maadili mema.
Matafi ameongeza kuwa, utamaduni pia unahamasisha jamii kuwa wamoja, wenye upendo, na kudumisha amani kwa kuishi bila vurugu.
Nao baadhi ya wanafunzi walioshiriki matembezi hayo, wamesema wamejifunza mambo mengi kuhusu utamaduni wa Kisukuma, ambao unawasaidia katika kudumisha amani, upendo, utulivu, na ushirikiano miongoni mwao.
Aidha, wananchi wote wanakaribishwa kushiriki kwenye Tamasha hilo ambalo ni bure hakuna kiingilio, kuanzia Julai 24 hadi 26, 2026 viwanja vya shule ya msingi Nhelegani.
TAZAMA PICHA👇👇
Msaidizi wa Chifu wa Utemi wa Kizumbi, ambaye pia ni Mwandaaji wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma mkoani Shinyanga,Peter Frank Lugumi (maarufu kama Mr Black), akizungumza.