Na Beda Msimbe, BSKY Media
Kiwango cha utumikishwaji wa watoto nchini Tanzania kimeshuka na kufikia asilimia 25.8 kwa mujibu wa taarifa ya Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi wa mwaka 2024, huku serikali ikipanga kuondoa kabisa tatizo hilo hadi kufikia asilimia sifuri ifikapo mwaka 2030.
Takwimu hizo zimebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mheshimiwa Deus Clement Sangu, katika taarifa yake kwa umma kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 12.
Waziri Sangu alieleza kuwa ili kufikia lengo hilo la mwaka 2030, serikali imebuni Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Mtoto wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30, unaohitaji ushiriki wa wananchi wote katika utekelezaji wake.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Kadi Nyekundu kwa Ajira ya Watoto; Haki sawa kwa Watoto, Kazi za Staha kwa watu Wazima,” ambayo inaenda sambamba na maendeleo na juhudi za nchi katika kupunguza idadi ya watoto wanaotumikishwa.
Waziri Sangu alifafanua kuwa utumikishwaji wa mtoto ni kitendo cha kikatili kinachowanyima watoto walio chini ya umri wa miaka 18 haki zao za msingi kama elimu, makuzi bora na malezi ya familia, jambo ambalo nchi imelikataza kisheria kupitia Kifungu cha Tano cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Sura 366.
Aliongeza kuwa kitendo hicho kina madhara makubwa kiuchumi kwani kinaharibu ndoto na vipawa vya watoto ambavyo vingesaidia familia zao, huku pia kikasababisha bidhaa zinazozalishwa kwa nguvu kazi ya watoto kukosa masoko barani Ulaya na duniani kote kutokana na kukiuka Kanuni za Umoja wa Mataifa za Biashara na Haki za Binadamu.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Tanzania imeweka mikakati thabiti kupitia Sera ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 inayozingatia haki za watoto na kupunguza uwezekano wa watoto chini ya miaka 17 kuingia kwenye kazi hatarishi, ambapo viongozi wa ngazi zote na wananchi wametakiwa kuhakikisha watoto waliopo umri wa kwenda shule hawaingizwi kwenye ajira. Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa ni pamoja na ushirikiano kati ya serikali na Sekta ya Kilimo kupitia ufadhili wa Shirika la ECLA, uliofanikisha uandishi wa Mwongozo wa Kazi katika Kilimo unaolenga kuzuia utumikishwaji wa watoto katika mnyororo wa thamani wa mazao.
Juhudi hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa na kufanikiwa kutokomeza kabisa utumikishwaji wa watoto katika kilimo cha Tumbaku, Mkonge, Chai na Pamba nchini.
Kutokana na mafanikio hayo, Waziri Sangu ametoa rai kwa wadau na makampuni ya sekta nyingine kama uvuvi, madini na biashara kuiga mfano huo kwa kuweka mikakati ya pamoja ya kutokomeza tatizo hilo, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kupinga utumikishwaji wa watoto kwa vitendo, pamoja na kushukuru mashirika ya ATE, TUCTA na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa ushirikiano wao endelevu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464