` RAIS SAMIA ATOA MAELEKEZO KUIMARISHA MAZINGIRA YA UTOAJI MIKOPO

WANDAMAN HOTEL

RAIS SAMIA ATOA MAELEKEZO KUIMARISHA MAZINGIRA YA UTOAJI MIKOPO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezielekeza Wizara ya Fedha, BoT na taasisi zote za fedha nchini kuimarisha mazingira ya upatikanaji wa mikopo, kupunguza gharama na riba, na kuongeza ushindani ili kunufaisha sekta binafsi, wanawake, vijana, wakulima na wafanyabiashara wadogo. 

Rais Samia alisisitiza kuwa mafanikio ya mfumo wa fedha yasipimwe kwa idadi tu ya wananchi waliofikiwa, bali kwa namna huduma hizo zinavyoongeza kipato, kupanua biashara, kutoa mitaji kwa wakati, na kusaidia vijana kuanzisha kampuni, huku akizitaka taasisi hizo kupitia upya vigezo vya utoaji mikopo kwa kuzingatia historia ya biashara na mauzo badala ya kutegemea dhamana za jadi pekee. 

Rais Samia alitoa maagizo hayo  katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yaliyofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Awali Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alisema kufikiwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunahitaji mageuzi makubwa ya sekta ya fedha yanayoendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na kiuchumi, huku Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, akibainisha kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kutoka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa mwaka 1994 hadi takriban asilimia 16 mwaka 2025, mikopo chechefu ikishuka hadi asilimia 2.9 mwezi Februari 2026, na akiba ya fedha za kigeni ikitosheleza zaidi ya miezi minne. 

Mafanikio hayo ya huduma jumuishi za kifedha, ubunifu wa kidijitali na mifumo ya malipo ya papo kwa papo nchini Tanzania yalisifiwa pia na Afisa Mtendaji Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (AFI), Dkt. Alfred Hannig, aliyetaja BoT kuwa miongoni mwa benki kuu zinazoongoza barani Afrika katika eneo hilo.

Katika hafla hiyo, Rais Samia pia alitunukiwa Tuzo Maalumu ya “Kinara wa Mageuzi ya Mifumo na Huduma Jumuishi za Kifedha”. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464