` WATUMISHI 14 WA TANESCO SHINYANGA WAKABILIWA NA MASHITAKA 10 YA UHALIFU

WANDAMAN HOTEL

WATUMISHI 14 WA TANESCO SHINYANGA WAKABILIWA NA MASHITAKA 10 YA UHALIFU

 


                                                    Na mwandishi wetu.

 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imewafikisha mahakamani watuhumiwa 14 ambao ni wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakikabiliwa na mashitaka 10 mbalimbali, ikiwemo kuunda genge la uhalifu, wizi unaofanywa na watumishi wa umma pamoja na kuisababishia Serikali hasara ya shilingi milioni 121.429.

Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga mbele ya Hakimu Mkazi, Yusuph Zahoro, ambapo upande wa mashtaka ulisoma mashitaka yanayowakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, Mwanasheria wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Martha Mbando, alisema uchunguzi wa shauri hilo umekamilika na sasa kesi ipo katika hatua za kuendelea na mchakato wa kimahakama.

Watuhumiwa waliopandishwa kizimbani ni Abdulkadir Lwasa, Fransis Mwasengo, Aisha Upete, Mugete Bernado, Noel Kale, Ibrahim Kiyungu, Monika Mpokwa, Faraja Ngao, Emanuel Matozi, Yusuph Mogaya, Saphia Jabu, Godwini Swai, Augustino Aloyce na John Gadi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo katika nyakati tofauti wakati wakitekeleza majukumu yao ya kikazi, hali iliyosababisha Serikali kupata hasara kubwa ya fedha.

Mahakama ilielezwa kuwa watuhumiwa wote 14 walishindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa, hivyo wakaamriwa kurejeshwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Juni 15, 2026, litakaporejea mahakamani kwa hatua nyingine za usikilizwaji.

Kesi hiyo imevuta hisia za wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kutokana na uzito wa tuhuma zinazowakabili watuhumiwa hao na athari zake kwa uchumi wa Serikali pamoja na utoaji wa huduma za umeme kwa wananchi.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464