Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, ametoa wito kwa Kanisa kuendelea kuwa nguzo muhimu ya kuhubiri amani, mshikamano na upendo katika jamii ili kuimarisha umoja wa wananchi na maendeleo ya Taifa.
Mwaselela ametoa kauli hiyo Juni 7, 2026 katika kanisa la KKKT Usharika wa Forest, jijini Mbeya, wakati wa maadhimisho ya miaka 46 ya huduma ya Kwaya Kuu Kongwe ndani ya kanisa hilo.
Akizungumza na waumini na viongozi wa dini, amesema kumtegemea Mungu kunamjenga mwanadamu kuwa na matumaini, maadili mema na mwelekeo sahihi wa maisha, hali inayochangia ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
"Jamii inayojengwa katika misingi ya upendo, mshikamano na kuheshimiana huendelea kuwa na utulivu na uwezo mkubwa wa kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali," amesema Mwaselela.
Aidha, amewahimiza viongozi wa dini na wazazi kuendelea kuwalea watoto katika maadili mema, hofu ya Mungu na uzalendo ili kujenga kizazi chenye nidhamu na uwajibikaji.
Pia amewataka waumini na Watanzania kwa ujumla kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kupata afya njema na hekima katika kuwatumikia wananchi na kuiongoza nchi kuelekea maendeleo zaidi.