
Katika jitihada za kuimarisha chachu ya maendeleo nchini, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Seneti Mkoa wa Mwanza umeandaa Kongamano la Wasomi lililofanyika Juni 7, 2026, katika Chuo cha Uvuvi Nyegezi, likiwa na lengo la kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa amani, umoja na mshikamano uliopo nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Vyuo na Vyuo Vikuu wa UVCCM Seneti Mkoa wa Mwanza, Kenneth Geremia, amewasisitiza vijana kuonyesha mapenzi ya dhati kwa taifa kwa kulinda amani, umoja na utulivu uliopo nchini.
Amesema vijana ndio wenye kuamua hatma ya taifa, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanaendelea kupatikana.
“Ninapenda kutoa wito kwa kila kijana kufanya uwajibikaji na uzalendo kuwa vipaumbele vyao vya kwanza katika ujenzi wa taifa, kwani vijana ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi,” alisema Geremia.
Aidha, amewahimiza vijana kujitolea kikamilifu katika shughuli za kijamii na kisiasa, akibainisha kuwa uwajibikaji thabiti ni msingi muhimu wa mafanikio ya taifa. Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa chachu ya maendeleo badala ya kutumiwa kama nyenzo za kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464