
Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA) yameleta fursa na changamoto kubwa nchini.
Licha ya kurahisisha maisha, teknolojia hii imekuwa na athari hasi kwa baadhi ya vijana ambao wamebweteka na kuacha kushughulisha miili na akili zao katika kazi halali.
Badala yake, wengi wanatumbukia kwenye uhalifu wa mitandaoni, udhalilishaji wa kijinsia, wizi wa fedha, na uraibu hatari wa michezo ya kubahatisha (kubeti) ambao unaletea hasara za kifedha na kuathiri afya zao za akili.
Kama nguvu kazi na tegemeo la taifa la kesho, vijana wengi wana ndoto kubwa za kuwa wafanyabiashara, wataalamu, au viongozi. Hata hivyo, changamoto kubwa ni tamaa ya kupata mafanikio ya haraka bila kupitia mchakato halali unaohitaji juhudi, nidhamu, na uwajibikaji.
Hali hii inawafanya warubuniwe kirahisi na wanasiasa wapenda vurugu kupitia mitandao ya kijamii, na kugeuzwa mateka wa kisiasa wanaosaliti tunu ya amani na uzalendo kwa kuahidiwa utajiri hewa.
Kwa mujibu wa Rehema Mwampamba, Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu wa fani ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC) uchunguzi unaonyesha kuwa vijana wengi wamepofushwa na teknolojia kiasi cha kupa kipaumbele mambo ya hovyo yanayohatarisha mustakabali wao na wa taifa, huku wakiahirisha mambo ya msingi yenye tija.
Tabia ya kukosa malengo na kuiga maisha ya wengine mtandaoni inawafanya kupoteza muda mwingi ambao ungepaswa kutumika kujifunza ujuzi mpya, kutangaza biashara, na kupata maarifa yatakayobadili maisha yao kiuchumi na kijamii.
Mwampamba anawaasa vijana kukataa kugeuzwa kuwa madaraja au zana za wanasiasa kufikia maslahi binafsi.
Badala yake, wanatakiwa kutumia TEHEMA kuongeza ufahamu, kushiriki mijadala chanya, na kulinda amani ya nchi. Teknolojia isitumiwe kama kisu cha kugawa jamii au jukwaa la kutukana viongozi, bali iwe fursa ya kujiajiri kwenye kilimo, masomo, na ubunifu.
Mwisho, mafanikio ya kweli yanajengwa hatua kwa hatua kwa misingi ya uadilifu na uzalendo.
Ili kufikia ndoto zao, vijana wanapaswa kuamka, kuacha kusubiri miujiza ya kubebwa, na kuchukua jukumu la maisha yao kwa kuweka malengo thabiti na kufanya kazi kwa bidii.
TEHEMA inatakiwa kuwa asali na chumvi ya kuijenga jamii, na si sumu ya kuiangamiza.