` RC SHINYANGA, AZINDUA MFUMO WA KIDITALI WA KUPOKEA TAARIFA ZA WANANCHI

WANDAMAN HOTEL

RC SHINYANGA, AZINDUA MFUMO WA KIDITALI WA KUPOKEA TAARIFA ZA WANANCHI

 


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita akizungumza na vyombo vya habari .

Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amezindua mfumo wa kidigitali utakaowezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za Serikali bila kulazimika kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Uzinduzi huo umefanyika leo Juni 17, 2026 katika Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ukiwa na lengo la kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wa Serikali mkoani humo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mhita amesema Serikali imeweka utaratibu wa kupokea malalamiko, kero, maoni na ushauri kutoka kwa wananchi kwa njia mbalimbali za kidigitali ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Amesema pamoja na ziara zinazofanywa na viongozi wa Serikali, ikiwemo wakuu wa wilaya na wakurugenzi ambao hukutana na wananchi katika siku maalum, mfumo huo mpya utaongeza fursa kwa wananchi kuwasilisha changamoto zao wakati wowote na kutoka mahali popote.

Mhe. Mhita ameeleza kuwa wananchi wanaweza kutumia njia mbalimbali kuwasilisha taarifa zao, ikiwa ni pamoja na:

-Kupiga Simu kwa Mkuu wa Mkoa kwa namba   0737 108 177ambayo iko WhatsApp,Barua pepe:rcshinyanga@go.tz na Mfumo wa E-Mrejesho wa serikal.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, mfumo wa E-Mrejesho utawasaidia wananchi kutoa maoni, kuuliza maswali, kuwasilisha malalamiko na kupendekeza maboresho ya huduma mbalimbali za Serikali.

Amesema mfumo huo umezingatia usiri wa taarifa za wananchi, hivyo mtoa taarifa anaweza kuwasilisha ujumbe wake bila kutambulika endapo atahitaji kufanya hivyo.

"Mwananchi anaweza kupiga simu au kuwasilisha taarifa wakati wowote. Masuala ya usalama na maendeleo ya Taifa ni jukumu la kila mmoja wetu," amesema Mhe. Mhita.

Aidha, wananchi wasiokuwa na bando la intaneti wanaweza kutumia huduma ya USSD kwa kupiga *152*00#, kisha kuchagua namba 03 na kufuata maelekezo yatakayowaongoza kupata huduma husika.

Mhe. Mhita amesema kauli mbiu ya mpango huo ni "Sema Usikike", ikiwa ni sehemu ya mkakati wa viongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha sauti za wananchi zinasikilizwa na changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Amesisitiza kuwa kila idara na kiongozi wa Serikali mkoani humo atawajibika kushughulikia malalamiko, maoni na mapendekezo yatakayowasilishwa kupitia mfumo huo ili kuimarisha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464