DC MTATIRO AZITAKA TIMU ZA WATAALAMU KUTATUA MIGOGORO YA WANANCHI KWA KUTENDA HAKI
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amezitaka timu za wataalamu zinazohusika na utatuzi wa migogoro kuhakikisha zinashughulikia kero za wananchi, kwa kuzingatia haki na kufuata taratibu ili kupata suluhisho la kudumu.
TAZAMA VIDEO👇👇
Mtatiro ametoa maagizo hayo leo Juni 17, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Tarafa ya Itwangi, uliofanyika katika Shule ya Msingi Didia wilayani Shinyanga.
Amesema kero zote zilizowasilishwa katika mkutano huo zinapaswa kushughulikiwa ndani ya siku 14, na kwamba wataalamu watakaopewa jukumu hilo wanapaswa kufanya kazi kwa umakini, weledi na kwa misingi ya haki.
“Mnapotatua migogoro ya wananchi, katendeni haki. nimeshawahi kutuma timu za halmashauri kwenda kutatua mgogoro, lakini ziliponiletea taarifa nikakataa kwa sababu hazikuwa zimetenda haki, nilifika mwenyewe eneo husika na kutatua mgogoro huo tofauti na walivyopendekeza, na hadi leo wananchi wanaishi kwa utulivu,” amesema Mtatiro.
Aidha, ameagiza pia katika utatuzi huo wa kero za wananchi, timu za wataalamu, wafike kwenye maeneo husika ya wananchi na utatuzi huo ufanyike pia kwa maandishi.
Katika mkutano huo, wananchi pamoja na Wenyeviti wa vijiji waliwasilisha kero mbalimbali zikiwamo migogoro ya ardhi na mipaka, masuala ya mirathi, ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa huduma za maji safi na salama pamoja na changamoto za upatikanaji wa umeme ngazi ya vitongoji.
Mtatiro ameahidi kuwa, serikali ya wilaya itaendelea kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo ili kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma bora kwa wakati.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa akizungumza.
Diwani wa Kata ya Ilola Kisena Kisena akizungumza.