` WATOTO SHINYANGA KUPATA HUDUMA MAALUM MASOKONI NA STEND

WANDAMAN HOTEL

WATOTO SHINYANGA KUPATA HUDUMA MAALUM MASOKONI NA STEND

 

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Thomas Sosoma akizungumza katika kikao cha mkoa cha kujadili malezi na makuzi ya watoto.

Na mwandishi wetu

SHINYANGA – Serikali imezielekeza Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Halmashauri ya Mji wa Kahama kuanza kutenga na kujenga maeneo maalum ya kulelea watoto katika masoko na stendi za mabasi ili kuimarisha ulinzi, malezi na makuzi ya watoto wadogo.

Maelekezo hayo yametolewa na Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Thomas Sosoma, wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kwa kipindi cha miezi sita kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ya mtoto mkoani Shinyanga.

Sosoma alisema kuwa uanzishwaji wa maeneo hayo maalum utasaidia kuhakikisha watoto wanaoambatana na wazazi au walezi wao katika shughuli za kiuchumi wanapata mazingira salama ya kucheza, kujifunza na kukua kwa maendeleo timilifu.

Alisisitiza kuwa uwekezaji katika malezi na makuzi ya watoto ni msingi wa kujenga taifa lenye rasilimali watu bora, hivyo akazitaka halmashauri, mashirika ya kiraia na wadau wengine kuendelea kuunga mkono afua zinazohusu maendeleo ya watoto wa umri wa miaka 0 hadi 8.

Aidha, aliwataka wamiliki wa vituo vya kulelea watoto mchana ambavyo bado havijasajiliwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Serikali ili kuhakikisha watoto wanapata huduma bora na salama zinazokidhi viwango vinavyotakiwa.

Pia aliwahimiza viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuendelea kutoa mafunzo ya maadili na imani kwa watoto pamoja na wazazi, akieleza kuwa malezi bora yanahitaji ushirikiano wa familia, jamii na taasisi mbalimbali.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lyidia Kwesigabo, amepongeza vyombo vya habari kwa mchango wake mkubwa wa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kupitia utekelezaji wa Programu ya PJT-MMMAM. Alisema ushiriki wa wanahabari umechangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa malezi bora, afya, lishe, ulinzi na ujifunzaji wa awali kwa watoto.

Kwesigabo amesema ofisi yake imeendelea kushauri mameneja wa masoko na stendi za mabasi kutenga maeneo ya madawati ya ustawi wa jamii ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Alieleza kuwa madawati hayo yatasaidia kutoa elimu, ushauri na huduma mbalimbali za ustawi wa jamii pamoja na kuimarisha ulinzi wa watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Programu wa Shirika la Investment in Children Society (ICS), Lucy Maganga, amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Programu ya PJMMAM inayolenga kuboresha afya, lishe, ujifunzaji wa awali, ulinzi na malezi yenye mwitikio kwa watoto.

Wadau kutoka sekta za afya, elimu, ustawi wa jamii, mashirika ya kiraia, vyombo vya usalama na viongozi wa jamii walishiriki kikao hicho kwa lengo la kutathmini mafanikio, changamoto na kuweka mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa programu hiyo kwa ustawi wa watoto na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Afisa ustawi wa Jamii mkoa wa Shinyanga,Lydia Kwesigabo akizungumza katika kikao cha malezi na makuzi cha mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya program ya PJTMMMAM.

Afisa Program wa shirika la ICS -ambao ni waratibu wa kitaifa wa program ya PJTMMMAM



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464