
Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa kiwanda cha Msumba Steel Tanzania Ltd kilichopo kata ya Mwendakulima Manispaa ya Kahama wakati wa hafla ya kusherekea mafanikio ya kiwanda hicho tangu kuanzishwa kwake nchini.
Mkurugenzi wa Musumba Steel Tanzania Ltd, Albert Uwiragiye akiendelea kufuatilia matukio mbalimbali wakati wa sherehe za kutambua mchango wa wafanyakazi wake
Katika kipindi ambacho juhudi za Serikali za kuimarisha uwekezaji, kukuza sekta binafsi na kuongeza ajira kwa vijana zinaendelea kushika kasi nchini, uongozi wa Kiwanda cha Musumba Steel kilichopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, umewataka wafanyakazi wake kudumisha mshikamano na ushirikiano ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho katika hafla maalum ya kutambua mchango wa watumishi, Mkurugenzi wa Musumba Steel, Albert Uwiragiye amesema umoja na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi ndiyo msingi mkuu wa mafanikio ya kampuni hiyo pamoja na maendeleo endelevu ya taasisi.
“Tunapaswa kutambua kuwa sisi ni ndugu tuliounganishwa na Musumba Steel, Ushirikiano wetu ndiyo nguvu ya kuifanya kampuni hii izidi kukua na kufikia malengo yake,” amesema Albert.
Aidha, amesema uwepo wa kiwanda hicho ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta binafsi ambayo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi kupitia utoaji wa ajira kwa vijana nchini, ambapo amewataka wafanyakazi kuzingatia kazi na kuepuka migogoro isiyo na tija ambayo inaweza kudhoofisha uzalishaji.
Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mafanikio ya Musumba Steel yanategemea kwa kiasi kikubwa juhudi na uzalendo wa wafanyakazi wake ambao wameendelea kuwa chachu ya uzalishaji na maendeleo ya kampuni hiyo.
Amesema tangu kuanzishwa kwake, kiwanda hicho kimefungua fursa nyingi za ajira kwa vijana wa Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga na maeneo mbalimbali nchini, hatua ambayo imechangia kuongeza kipato kwa wananchi pamoja na kuboresha maisha yao.
Pia ameishukuru menejimenti na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kujituma na kuwa sehemu ya mafanikio makubwa ambayo Musumba Steel imeendelea kuyapata katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake.
Kwa upande wake, Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho, Halfan Shaibu amesema kampuni hiyo imepiga hatua kubwa katika uzalishaji tangu ilipoanza rasmi shughuli zake mwaka 2022.
Amesema uwepo wa kiwanda hicho umeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa eneo la Kahama na maeneo ya jirani, huku akiwapongeza wafanyakazi kwa kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya kampuni hiyo.
Naye Meneja wa Usafirishaji na Manunuzi, Diodone Ndereyikumana amesema jukumu la kila mfanyakazi ni kuhakikisha kampuni inaendelea kusonga mbele huku uzalishaji ukiongezeka siku hadi siku.
“Bila wafanyakazi, kiwanda si kitu. Tunapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kutokata tamaa katika utekelezaji wa majukumu yetu,” amesema Diodone.
Katika kuhamasisha utendaji kazi wenye tija, Mkurugenzi wa Musumba Steel ametoa zawadi kwa wafanyakazi bora wanne waliotambuliwa kwa kufanya vizuri katika majukumu yao tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho mwaka 2022.
Kiwanda cha Musumba Steel Tanzania Limited kilianzishwa rasmi mwaka 2022 na kinajihusisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo mabati, misumari, square pipe pamoja na round pipe, kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi wa Kahama, Shinyanga na maeneo ya Kanda ya Ziwa badala ya kutegemea bidhaa kutoka jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Musumba Steel Tanzania Ltd
sehemu ya kiwanda cha Musumba Steel Tanzania Ltd
Mkurugenzi wa Musumba Steel Tanzania Ltd, Albert Uwiragiye akisalimiana na viongozi mbalimbali wa kiwanda hicho .
Bw. Andrea Samwel Meneja Mradi kiwanda cha Musumba Steel Tanzania Ltd.
Halfan Shaibu Mkuleje-Meneja uzalishaji kiwanda cha Musumba Steel Tanzania Ltd.
Deus Wambwe -Meneja Mauzo na Masoko Kkiwanda cha Musumba Steel Tanzania Ltd
Meneja wa Usafirishaji na Manunuzi, Diodone Ndereyikumana
Bw. Andrea Samwel Meneja Mradi kiwanda cha Musumba Steel Tanzania Ltd.
Didace Tuyizingire -Meneja Fedha
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464