` WANANDOA SHINYANGA WAHAMASISHWA KUMILIKI HATI ZA PAMOJA KUEPUSHA MIGOGORO YA MIRATHI

WANDAMAN HOTEL

WANANDOA SHINYANGA WAHAMASISHWA KUMILIKI HATI ZA PAMOJA KUEPUSHA MIGOGORO YA MIRATHI

 


Wanandoa mkoani Shinyanga wamehimizwa kuhakikisha wanamiliki hati za ardhi kwa pamoja kama njia ya kulinda haki za familia na kuepusha migogoro ya mirathi inayoweza kujitokeza baada ya mmoja wa wanandoa kufariki dunia.

Wito huo umetolewa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Shinyanga, Bw. Leo Komba, wakati wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea katika Manispaa ya Shinyanga, ikiwa na lengo la kuwahudumia wananchi katika masuala mbalimbali ya kisheria hususan sekta ya ardhi.
Bw. Komba amesema kuwa umiliki wa hati za pamoja kwa wanandoa husaidia kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi ndani ya familia pamoja na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza baina ya wanafamilia au warithi baada ya kifo cha mmoja wa wanandoa.

Aidha, amefafanua kuwa mchakato wa kupata hati ya umiliki wa pamoja hautofautiani na ule wa hati ya mtu mmoja, ikiwemo upande wa gharama, mradi tu wanandoa wamekubaliana kumiliki ardhi hiyo kwa pamoja.

“Ni muhimu kwa wanandoa kutambua kuwa umiliki wa pamoja unasaidia kulinda haki za kila upande na kuimarisha amani ndani ya familia,” amesema Bw. Komba.

Kwa upande wao, Richard Magezi na Frola Manyangu ambao ni miongoni mwa wanandoa waliopatiwa huduma ya hati ya umiliki wa pamoja kupitia kampeni hiyo, wameeleza kuwa hatua hiyo itawasaidia kuepusha migogoro ya ardhi na kuimarisha usalama wa mali za familia yao siku zijazo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464