` UCHAMBUZI: JOHN MNYIKA ACHEMKA, VIJANA WAZALENDO WAGOMEA HADAA NA UPOTOSHAJI WA KISIASA

UCHAMBUZI: JOHN MNYIKA ACHEMKA, VIJANA WAZALENDO WAGOMEA HADAA NA UPOTOSHAJI WA KISIASA

Serikali ya Awamu ya Sita imetoa wito mzito kwa vijana nchini kote kuwa macho na kuepuka kusikiliza maneno ya hadaa yanayolenga kuwapotosha, ikisisitiza kuwa imejipanga kikamilifu kuwaendeleza kiuchumi na kijamii kupitia mipango madhubuti inayotekelezeka kwa vitendo.

 Katika kuhakikisha ustawi wa vijana unakuwa kipaumbele, uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuunda Wizara mahususi ya Vijana umetajwa kama kielelezo tosha cha utayari wa serikali katika kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili vijana kote nchini. 

Hatua hii imeenda mbali zaidi kwa kuimarisha mifumo ya kujiendeleza kiuchumi ikiwemo utoaji wa mikopo ya asilimia kumi inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ambayo inawapa vijana mitaji ya kuanzisha biashara, sambamba na programu kabambe za uanagenzi zinazowapa stadi na maarifa ya kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika soko la ajira.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni jibu la moja kwa moja kwa wapinzani, madai ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, yanayodai uwepo wa hadaa ndani ya serikali kwa kuunda wizara ya vijana yamepingwa vikali na kutajwa kuwa ni hoja mufilisi zisizo na msingi wowote wa kisheria wala kiuhalisia. 

Serikali imebainisha kuwa uongozi uliopo ni halali, umechaguliwa na wananchi kwa kura nyingi, na unafanya kazi kwa kutumia takwimu zinazoonekana badala ya maneno matupu ya kisiasa. 

Imesisitizwa kuwa kiongozi huyo amechemka kwa sababu kila hatua ya maendeleo inayopigwa hivi sasa inajionyesha yenyewe kupitia miradi mikubwa na takwimu za ukuaji wa uchumi zinazogusa maisha ya vijana moja kwa moja, jambo linalomhitaji Mnyika kutafuta mada nyingine badala ya kupotosha umma.

Kauli zake hizo zipo katika video mitandaoni ambapo kiongozi huyo wa CHADEMA anaonekana akitaja kuhusika kwa vijana wa chama chake katika vurugu zilizotokea Oktoba 29, na kueleza kwamba uundaji wa wizara ni hadaa. 

Mijadala katika kurasa mbalimbali za kijamii kama kaka_wataifa_tz na wakazi_tv inaonyesha wananchi wakihoji uhalali wa chama hicho na kauli zake ambazo zinaonesha wao kuwa kikwazi katika maendeleo ya taifa hili kwa kuchochea vurugu.

Kutokana na mazingira haya, serikali imesisitiza kuwa kuwapo kwa wizara hiyo si hadaa na kuwataka vijana kusisitiza amani ili fursa kuu zilizopo ziweze kuwainua vijana na kujijenga kimaarifa na kiuchumi badala ya kukubali kutumika katika vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo havina tija yoyote kwa mustakabali wa taifa lao. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464