` AMANI NDIO NGAO: SERIKALI NA JMAT ZASISITIZA MARIDHIANO KUANZIA NGAZI YA FAMILIA

AMANI NDIO NGAO: SERIKALI NA JMAT ZASISITIZA MARIDHIANO KUANZIA NGAZI YA FAMILIA

Serikali imetoa wito mzito kwa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kuelekeza nguvu zake katika kutibu migogoro ya kijamii kuanzia ngazi ya familia ili kurejesha furaha na mshikamano wa kitaifa ambao ndio msingi mkuu wa maendeleo. 

Katika mikutano iliyofanyika kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam na wilayani Mkuranga mkoani Pwani, viongozi wa serikali na wadau wa amani wamebainisha kuwa utulivu wa nchi si suala la hiari bali ni hitaji la lazima katika kuvutia uwekezaji na kuhakikisha wananchi wanafanya kazi zao bila hofu. 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameitaka JMAT kuwa daraja imara la kusaidia serikali kutatua kero za mirathi, migogoro ya ardhi, na ukatili wa kijinsia, akisisitiza kuwa amani ya kweli inajengwa kuanzia ngazi ya chini kabisa ambapo jamii inahitaji huduma na maelewano.

Mwenyekiti wa JMAT Taifa, Shehe Alhad Mussa Salum, amepokea wito huo kwa kuahidi kuwa jumuiya yake haitayumba katika kulinda amani ya nchi na ndiyo maana wameamua kuanzisha idara mpya za wazee, wanawake, na vijana ili kuongeza nguvu ya maridhiano nchini kote. 

Hoja hiyo ya amani imeungwa mkono na wadau huko Mkuranga ambapo amani imetajwa kama ngao ya nchi inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote dhidi ya makundi yanayolenga kuwagawa wananchi. 

Mkurugenzi wa African Talent Forum, Rosemary Bujashi, amewataka Watanzania kuacha kujiingiza kwenye makundi yanayoyumbisha nchi, huku Mwenyekiti wa JMAT Mkuranga, Shukuru Ngweshani, akisisitiza kuwa utulivu na mshikamano ndiyo jadi ya pekee itakayolifanya taifa lisonge mbele kwa haraka zaidi.

Kumbukumbu za machafuko ya Oktoba 29, 2025, zimetajwa na wananchi kama fundisho tosha la kwanini amani inapaswa kuenziwa, ambapo wakazi kama Swaumu Nyungulu wameeleza adha waliyoipata wakati shughuli za kiuchumi na masomo ziliposimama. 

Wananchi Clinton Gidion na Witness Lema wameongeza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuepuka ubaguzi na uchochezi, huku wakihimiza mazungumzo ya staha kama njia ya kutatua tofauti zilizopo. 

Diwani wa Kata ya Mkuranga, Hamza Mahanaka, amehitimisha kwa kutoa rai kwa vijana kujiepusha na makundi yanayoweza kuharibu sifa ya nchi, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuhubiri upendo ili kuvutia wawekezaji na kuruhusu uzalishaji kuendelea kwa ajili ya ustawi wa kila Mtanzania.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464