.jpg)
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limegeuka kuwa jukwaa la matumaini kwa vijana nchini kufuatia wabunge na viongozi wa serikali kuainisha fursa kemkem zilizowekwa ili kukuza uchumi wa kizazi hicho.
Akichangia mjadala wa hotuba ya Rais wakati wa ufunguzi wa Bunge la kumi na tatu, Mbunge wa Bunda Mjini, Mheshimiwa Ester Bulaya, amewahimiza vijana nchini kuchangamkia fursa zinazoletwa na serikali ya awamu ya sita akibainisha kuwa utekelezaji wa ahadi kubwa za Rais kuelekea kundi hilo tayari umeanza kwa vitendo.
Mheshimiwa Bulaya amefafanua kuwa miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanyika ni uamuzi wa Rais kutoa kipaumbele kwa vijana katika wizara zote pamoja na kutenga kiasi cha shilingi bilioni mia mbili kwa ajili ya vijana wajasiriamali nchini kote.
Aidha, amebainisha kuwa serikali imejikita katika kuwajengea vijana mazingira bora ya kufanya biashara na kuanzisha kampasi za vyuo katika maeneo mbalimbali ili kuwaandaa kitaaluma na kiufundi ili waweze kunufaika na fursa zinazojitokeza katika sekta ya viwanda inayokua kwa kasi.
Naye Mbunge wa Makete, Mheshimiwa Festo Sanga, amesisitiza umuhimu wa vijana kuendelea kuiunga mkono serikali na kulinda amani ya taifa, akieleza kuwa serikali ya sasa imefanya mabadiliko makubwa katika taasisi zake ili kuhakikisha changamoto za vijana zinatafutiwa suluhu ya kudumu.
Sanga amebainisha kuwa uwepo wa utulivu wa kisiasa na usimamizi wa misingi ya amani ni kichocheo muhimu kitakachowezesha ahadi na mikakati yote iliyopangwa na Rais Samia kumnufaisha mwananchi mmoja mmoja, hususan kijana aliyeko mitaani na vijijini.
Kwa upande wa teknolojia na habari, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Daktari Switbert Mkama, ameeleza bungeni kuwa serikali imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha gharama za vifurushi vya mtandao zinakuwa rafiki kwa kila Mtanzania.
Daktari Mkama amebainisha kuwa kupitia majadiliano na watoa huduma, Tanzania sasa imekuwa nchi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na huduma za intaneti za bei nafuu, hatua inayolenga kuchochea ubunifu na kusaidia vijana kutumia mtandao kujitengenezea fursa za kiuchumi na kijamii.
Maendeleo hayo ya kiteknolojia yameambatana na ujenzi wa minara ya mawasiliano na vituo vya kuhifadhi data nchini, hali inayosaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni za simu na hivyo kuwafanya wananchi kupata vifurushi vinavyokidhi uwezo wao.
Hali hii ya kuimarika kwa miundombinu ya mawasiliano ikichanganywa na uwekezaji wa mabilioni ya fedha katika sekta ya ujasiriamali, inatoa taswira ya nchi iliyojipanga kuhakikisha vijana wake wanakuwa sehemu kuu ya injini ya ukuaji wa uchumi wa kitaifa kuelekea malengo ya dira ya maendeleo ya taifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464