
Mageuzi makubwa ya kimkakati yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) yameleta mapinduzi ya kihistoria katika ukusanyaji wa mapato ya Forodha, hatua ambayo sasa imepata utambuzi wa juu kutoka kwa Shirika la Forodha Duniani (WCO).
Katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam Januari 26,2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bwana Plasduce Mbossa, ametunukiwa Cheti cha Heshima kutoka Shirika hilo la kimataifa kwa usimamizi wake thabiti uliowezesha ufanisi wa kipekee wa huduma za bandari kwa jumuiya ya kimataifa.Ufanisi huo wa bandari umekuwa chachu ya kuimarika kwa uchumi ambapo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bwana Yusuph Mwenda, amebainisha kuwa makusanyo kupitia idara ya forodha yamepaa kwa kasi na kufikia shilingi trilioni moja nukta mbili kwa mwezi, ikilinganishwa na wastani wa shilingi bilioni 800 uliokuwa ukikusanywa hapo awali.
Kamishna Mwenda ameielezea TPA kama mdau muhimu na mfano wa kuigwa ambaye kupitia uboreshaji wa mifumo yake na weledi katika utendaji, imesaidia kurahisisha biashara na kuimarisha udhibiti wa mapato ya serikali kwa kiwango cha juu.
Ongezeko hili la mapato ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa serikali katika teknolojia ya kisasa ya ukaguzi, ikiwemo ununuzi wa skana maalumu hamsini na saba zenye thamani ya dola za Marekani milioni tisini zilizofungwa mipakani na bandarini.
Aidha matumizi ya mifumo ya kidijitali kama TANCIS yameongeza uwazi na kupunguza urasimu, jambo ambalo limefanya Bandari za Tanzania kuwa lango salama na la kuaminika kwa biashara ya kimataifa, huku yakidhibiti uingizwaji wa bidhaa hatarishi na haramu nchini.
Akipokea tuzo hiyo ya kimataifa, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bwana Plasduce Mbossa, ameishukuru serikali kwa utashi wake wa kufanya mageuzi hayo na kuahidi kuwa heshima hiyo itakuwa hamasa ya kuendelea kuboresha huduma.
Amesitiza kuwa TPA itaendelea kuwekeza katika teknolojia na kuimarisha misingi ya uwajibikaji ili kuhakikisha bandari zinachangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa taifa na kulinda jamii, ikienda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu inayosisitiza umakini na uwajibikaji katika sekta ya forodha.
Utambuzi huu kutoka Shirika la Forodha Duniani ni dhihirisho tosha kuwa dunia inatambua na kuthamini mabadiliko chanya yaliyofanywa katika sekta ya bandari nchini Tanzania.
Pia ushirikiano madhubuti kati ya TPA na TRA unathibitisha kuwa mwelekeo wa sasa wa serikali katika kuimarisha miundombinu na mifumo ya forodha ni nguzo imara inayofanikisha malengo ya kimaendeleo na kuimarisha usalama wa biashara katika anga za kimataifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464