` MV NEW MWANZA: MKOMBOZI WA UCHUMI NA BIASHARA KANDA YA ZIWA

MV NEW MWANZA: MKOMBOZI WA UCHUMI NA BIASHARA KANDA YA ZIWA

Kukamilika na kuzinduliwa kwa meli ya kisasa ya MV New Mwanza, kumeleta matumaini mapya ya kiuchumi kwa mamilioni ya wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafirishaji wa bidhaa na abiria kati ya majiji ya Mwanza na Bukoba.

Meli hiyo, ambayo sasa ndiyo mfalme wa maji katika Ukanda wa Maziwa Makuu, si chombo cha usafiri tu, bali ni kiunganishi kikuu cha biashara kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Uganda na Kenya.

Uwezo wa Kipekee: 

Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu cha "ukame" wa vyombo vikubwa, MV New Mwanza inakuja na uwezo mkubwa wa kubeba abiria na mizigo. Ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 inapunguza msongamano na gharama kubwa za usafiri wa barabara.

Kwenye suala la mizigo ambapo ndipo penye moyo wa biashara, meli hii ina uwezo wa kubeba tani 400 za bidhaa kwa wakati mmoja, jambo ambalo litaleta mapinduzi ya bei za bidhaa sokoni. Aidha ina uwezo wa kubeba magari madogo 20 na makubwa (malori) 3 .

Manufaa ya Kiuchumi:

Kukosekana kwa meli ya uhakika kwa miaka mingi kuliathiri vibaya mabadilishano ya bidhaa. Sasa, kwa safari ya saa 6 hadi 7 pekee wakulima wa kahawa, ndizi, na mazao mengine ya chakula kutoka mkoani Kagera sasa wanakuwa na soko la uhakika jijini Mwanza na mikoa mingine.

 Bidhaa hizi zitafika zikiwa bado mbichi na kwa gharama nafuu ya usafirishaji.Wakati huo huo wafanyabiashara wa Mwanza sasa wanaweza kusafirisha bidhaa za viwandani, vifaa vya ujenzi, na samaki kwenda Bukoba na maeneo ya pembezoni mwa ziwa kwa urahisi zaidi.

Ongezeko la uwezo wa kubeba mizigo mikubwa kutaondoa gharama za ziada za usafirishaji zinazosababishwa na malori, hivyo kupelekea bei za bidhaa kupungua kwa mlaji wa mwisho.

Usalama na Utimamu wa Biashara 

Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Eric Hamisi, amebainisha kuwa meli hiyo imetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa inayohakikisha usalama wa watu na mali zao. Uwepo wa madaraja mbalimbali, ikiwemo daraja la biashara na VIP, unatoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya safari zao kwa faraja huku wakiratibu mipango yao ya kibiashara.

Kwa wakazi wa kandoni mwa Ziwa Victoria, MV New Mwanza si tu fahari ya kitaifa, bali ni injini ya kukuza kipato, kutoa ajira, na kufungua fursa za kitalii ambazo zilikuwa zimefifia. Huu ni mwanzo wa zama mpya ambapo biashara itashamiri na uchumi wa kaya utaimarika kupitia maji ya ziwa hilo kuu. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464