.jpg)
Uamuzi wa taasisi ya Gatsby Africa kufanya kazi nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 25 sasa unatokana na misingi imara ya utulivu wa kisiasa na diplomasia ya kiuchumi ambayo nchi imeendelea kuijenga na kuistawisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Gatsby, Justin Highstead, amebainisha kuwa Tanzania inamiliki mazingira rafiki ya uwekezaji na utashi mkubwa wa kisiasa wa kukubali mabadiliko, jambo linaloifanya nchi hii kuwa kama shamba darasa la mageuzi ya kiuchumi katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Utulivu wa muda mrefu uliopo nchini umekuwa kichocheo kikubwa kwa taasisi hiyo kuweza kupanga mipango ya kimkakati ya muda mrefu, inayochukua kati ya miaka kumi hadi ishirini, bila kuwa na hofu ya kuingiliwa na machafuko au mabadiliko yasiyotabirika.
Hali hii inatoa fursa ya pekee ya kuangazia rasilimali zilizolala, hususani katika sekta za viwanda na nishati, ambazo zikiguswa na sayansi pamoja na teknolojia ya kisasa, zinatarajiwa kuleta matokeo makubwa na chanya kwa uchumi wa taifa.
Kupitia majadiliano hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, imebainika kuwa ushirikiano huu utazaa matunda mengi ikiwemo kuongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha ushindani wa viwanda vya ndani ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Katika mazungumzo hayo kati ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, na Mkurugenzi Mtendaji wa Gatsby Africa, Justin Highstead, maeneo makuu matatu ya mageuzi ya viwanda, uwekezaji wa rasilimali fedha, na ujenzi wa rasilimaliwatu yenye ujuzi wa kisasa yaliguswa.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesisitiza kuwa uwekezaji huo unaenda sambamba na ujenzi wa rasilimaliwatu wenye ujuzi, utafutaji wa rasilimali za utekelezaji, na matumizi ya tafiti makini ambazo zimekuwa zikifanywa kwa ushirikiano na Tume ya Mipango.
Gatsby Africa ni nini?
Kwa wasiofahamu, Gatsby Africa ni taasisi ya kimaendeleo (charitable foundation) iliyoanzishwa na familia ya Lord Sainsbury nchini Uingereza. Tofauti na mashirika mengine ya misaada, Gatsby haitoi chakula au msaada wa dharura; badala yake, inafanya kazi ya "Market Transformation" (Mageuzi ya Masoko).
Kazi yao kubwa ni kushirikiana na Serikali kufanya utafiti wa kina, kuleta teknolojia, na kufungua mifumo ya kiuchumi ili sekta kama kilimo, misitu, na viwanda ziweze kujiendesha kwa ushindani wa kimataifa na kutengeneza ajira za kudumu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464