` MANISPAA YA SHINYANGA YAJA NA MKAKATI WA KUONGEZA MAPATO YA NDANI,MEYA ASISITIZA USHIRIKIANO

MANISPAA YA SHINYANGA YAJA NA MKAKATI WA KUONGEZA MAPATO YA NDANI,MEYA ASISITIZA USHIRIKIANO

 

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani 
Suzy Butondo,Shinyanga

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo amesema manispaa ya Shinyanga ina mpango wa kuboresha mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya upotevu pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuinua uchumi wa Manispaa na kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hayo ameyasema kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kilichofanyika kwenye ukumbi wa manispaa ya Shinyanga ambapo amesema manispaa ina mpango wa kudhibiti mapato pamoja na kubuni vyanzo vipya.

"Niwaombe madiwani wenzangu na wataalamu ili tuweze kukuza uchumi wetu ni vizuri tukashirikiana kwa pamoja katika kudhibiti mapato pamoja na kubuni mbinu mbalimbali ambazo zitasaidia kuongeza mapato ya manispaa,"amesema Kitumbo.
"Na haya yote tutayasimamia vizuri katika awamu hii na kuhakikisha kila kona ya manispaa tunaweka kitega uchumi ambacho kitaongeza kipato kwa manispaa na wananchi,"ameongeza Kitumbo

Aidha madiwani wa kata zote 17 za manispaa waliwasilisha taarifa zao na wakaomba changamoto zilizopo katika maeneo yao zitatuliwe kwa wakati na kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi katika maeneo yake.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Anold Makombe amewaomba madiwani kwenda kutekeleza kazi za wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi ili kuzitatua.

"Kwanza niwapongeze sana kwa kutoa mikopo kwa wananchi, nimefarijika sana sana kuona wananchi wanapatiwa mikopo, niwaombe tu kwa fedha zilizobaki muangalie uwiano kwenye kata zetu,pia maafisa wahamasisheni wanawake watu wenye ulemavu kwenye Kata zote huko mwamalili Kolandoto ,ili nao waje wanufaike na mikopo hii,"amesema Makombe.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Peres Kamugisha amesema maagizo yote yaliyotolewa na madiwani watayafanyia kazi na watashirikiana na madiwani wa kata husika, pale panapoonekana kuna changamoto ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani
Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Pendo Sawa








Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464