` RC MHITA AWASIHI WANANCHI SHINYANGA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE,KUPATA HUDUMA BORA ZA MATIBABU

RC MHITA AWASIHI WANANCHI SHINYANGA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE,KUPATA HUDUMA BORA ZA MATIBABU

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amewasihi wananchi wa mkoa huo kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ili waweze kupata huduma bora, nafuu na endelevu za matibabu kwa kipindi cha miezi 12.

Mhita ametoa wito huo leo Januari 30, 2026, wakati wa mkutano wa kuhamasisha kujiunga wa mpango wa bima ya afya kwa wote uliofanyika mkoani humo, ukihusisha viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali, viongozi wa dini, wananchi na makundi maalumu yakiwamo watu wenye ulemavu na wazee.
Amesema, serikali imeanza rasmi zoezi la usajili wa Bima ya Afya kwa Wote kuanzia Januari 26 mwaka huu, ambapo kaya yenye watu sita italipia Sh.150,000 sawa na Sh.25,000 kwa mtu mmoja na kupata huduma bora za matibabu kwa mwaka mzima.

Mhita amebainisha kuwa, mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora na endelevu za afya bila vikwazo vya kifedha.
“Kila Mtanzania atakayejiunga na Bima ya Afya kwa Wote atanufaika na huduma za afya ikiwamo huduma za kibingwa na bobezi kwa gharama nafuu. Kaya yenye watu sita italipia Sh.150,000 tu na kupata matibabu kwa mwaka mzima,” amesema Mhita.

Aidha, ameziagiza taasisi za umma na binafsi mkoani humo, kuhakikisha zinawaunganisha watumishi wao katika mpango huo wa bima, ili waweze kupata huduma bora za matibabu wanapokumbwa na changamoto za kiafya.
Akizungumzia wananchi wasiojiweza, Mhita amesema serikali itawalipia gharama za bima, akieleza kuwa tayari watu 63,450 wametambuliwa mkoani Shinyanga kufaidika na mpango huo.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, utasaidia pia kupunguza vifo, ambapo wananchi watakuwa na fursa ya kupima afya zao mara kwa mara, kupata ushauri wa kitaalamu na kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa bila kugharamika zaidi.

“Bima hii ya afya kwa wote ni mkombozi mkubwa wa afya kwa jamii,” amesema Mhita.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Shinyanga Isack Katenda, amesema utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ni wa lazima, na utamwezesha mwananchi kupata huduma bora za afya kuanzia ngazi ya zahanati, hospitali za wilaya, rufaa hadi hospitali za kibingwa.

Katenda amesema, zoezi la kuwasajili wananchi wasiojiweza litaanza Jumanne ijayo, ambapo watapita katika halmashauri zote za mkoa huo kuwasajili watu 63,450 waliotambuliwa kwa awamu ya kwanza.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Emmanuel Ruben, amesema mpango huo wa bima ya afya kwa wote ni kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa usawa za matibabu.
Nao baadhi ya washiriki wa mkutano huo wameipongeza serikali kwa kuanzisha mpango wa bima ya afya kwa wote, wakisema utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu kwa wananchi. hata hivyo, wameshauri zoezi la utambuzi wa kaya zisizojiweza lifanyike kwa ufanisi ili kuwafikia walengwa waliokusudiwa.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Emmanuel Ruben, akizungumza.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Shinyanga Isack Katenda akizungumza.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita (kushoto)akiwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464