` MAGEUZI YA RAIS SAMIA: MITI MILIONI MIA MOJA NA FURSA MPYA KWA VIJANA

MAGEUZI YA RAIS SAMIA: MITI MILIONI MIA MOJA NA FURSA MPYA KWA VIJANA

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetangaza mafanikio makubwa katika uhifadhi wa mazingira ambapo jumla ya miti 113,199,000 imepandwa nchi nzima ndani ya kipindi cha miaka mitatu. 

Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, amebainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano kati ya wakala huo na Shirika la Utangazaji Tanzania kupitia kampeni ya 27 ya kijani, ambayo inalenga kuhamasisha jamii kurejesha uoto wa asili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Profesa Silayo ameeleza kuwa katika kuitikia wito wa Rais wa kuhifadhi mazingira, jumla ya miche ya miti zaidi ya milioni 46  iligawiwa kwa wananchi ili ipandwe katika maeneo yao, huku miche mingine zaidi ya milioni 66 ikipandwa katika hifadhi za misitu na mashamba ya serikali kote nchini. 

Juhudi hizi zinatajwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ambaye Januari 27 ameongoza zoezi la kupanda miti kule Zanzibar kama ishara ya shukrani na utekelezaji wa wajibu wa kulinda maliasili za taifa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Sambamba na mafanikio hayo ya kimazingira, wadau wa maendeleo ya vijana wameeleza kuwa uongozi wa Rais Samia umeleta mageuzi makubwa yaliyofungua milango ya ajira na uwezeshaji wa kiuchumi kwa kizazi cha sasa.

 Mratibu wa Taasisi ya Together for Samia, Gulatone Masiga, amebainisha kuwa ujenzi wa vyuo vya ufundi na ujuzi katika wilaya zaidi ya 62 nchini umekuwa msaada mkubwa kwa vijana kupata maarifa ya vitendo yanayowawezesha kujiajiri. 

Ameongeza kuwa mabadiliko ya mtaala wa elimu yanayolenga kutoa stadi za kazi na uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati ni hatua zilizochochea ukuaji wa viwanda na biashara zinazowahusisha vijana moja kwa moja.

Aidha, hali ya mazingira ya biashara nchini imeelezwa kuendelea kuimarika ambapo vijana wengi wameanza kusajili biashara zao rasmi kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kutokana na sera rafiki zilizowekwa. 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana Innovations, Dorcas Mshiu, amepongeza mkakati maalum wa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia nne kwa vijana, akisisitiza kuwa hatua hiyo imekuwa mkombozi kwa wajasiriamali chipukizi wanaotaka kukuza mitaji yao. 

Hatua hizi kwa pamoja zinaonesha kuwa juhudi za utunzaji wa mazingira na uwekezaji kwa binadamu zinaenda sambamba katika kuiletea Tanzania maendeleo endelevu na jumuishi. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464