
Katika jitihada za kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani, serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepiga hatua kubwa kwa kuzindua mfumo wa kidijitali unaotumia Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) ujulikanao kama Bwana Bumu na Bibi Bumu.
Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma mnamo Januari 28, 2026, si tu tukio la kitaluma, bali ni ukombozi kwa maelfu ya vijana wanaokabiliwa na changamoto za kifedha katika masomo yao.Kwa kijana anayesoma, mfumo huu unamaanisha mwisho wa milolongo mirefu na kusubiri majibu kwa muda mrefu. Kupitia teknolojia ya Akili Unde, mfumo wa Bwana Bumu na Bibi Bumu una uwezo wa kuchakata taarifa kwa haraka na usahihi wa hali ya juu.
Hii inamaanisha kuwa mwanafunzi anaweza kupata majibu ya kero zake au taarifa za mkopo wake papo hapo bila kuhitaji kufika ofisi za bodi au kusubiri barua pepe kwa siku kadhaa.
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa HESLB, Bahati Singa, amebainisha kuwa mfumo huu umeunganishwa moja kwa moja na mifumo ya mikopo ya bodi, hivyo kutoa huduma inayozingatia taarifa halisi za mwanafunzi.
Kabla ya mfumo huu, bodi ilikuwa na uwezo wa kuwafikia wanufaika elfu tano hadi elfu sita tu kwa wakati mmoja, lakini sasa uwezo huo umepaa na unatarajiwa kuwafikia walengwa kati ya laki moja hadi laki mbili. Hii ni hatua kubwa itakayohakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma kwa kukosa taarifa.
Moja ya shida kubwa iliyokuwa ikiwakabili vijana ni kukwama kwa huduma nyakati za usiku, wikendi, au sikukuu. Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bili Kiwia, amesisitiza kuwa mfumo huu wa AI utakuwa ukitoa huduma saa 24 kwa siku saba za wiki, mwaka mzima.
Hii ina maana kwamba mwanafunzi anayehitaji msaada akiwa chuoni saa nane usiku anaweza "kuchati" na Bwana Bumu au Bibi Bumu na kupata muongozo wa haraka.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza malalamiko kwa kiasi kikubwa kwani mwanafunzi anakuwa na "ofisa mikopo" mfukoni mwake kupitia simu ya mkononi au kompyuta wakati wowote.
Serikali imejivunia kuwa mfumo huu umesanifiwa na wataalamu wazalendo wa ndani ya nchi, jambo linaloashiria kuwa nguvukazi ya Kitanzania ina uwezo wa kutatua matatizo ya nyumbani kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Kwa upande wa serikali na walipa kodi, matumizi ya mfumo huu ni ushindi mkubwa wa kiuchumi. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia hii yatapunguza gharama za utoaji wa huduma kwa takribani asilimia 60.
Gharama hizi zinazookolewa zinaweza kuelekezwa katika kuongeza idadi ya wanufaika au kuboresha maeneo mengine ya elimu.
Zaidi ya kutoa huduma, Bwana Bumu na Bibi Bumu wanakuja kuimarisha uwazi. Mfumo huu utawajengea wadau uelewa mpana kuhusu shughuli zote za bodi na jinsi mikopo inavyotolewa.
Hii inaondoa dhana ya upendeleo au usiri uliokuwa ukilalamikiwa huko nyuma. Aidha, wito umetolewa kwa wazazi na walezi kutobaki nyuma; wanapaswa kujifunza na kuutumia mfumo huu ili waweze kufuatilia maendeleo ya mikopo ya watoto wao na kupata taarifa sahihi kwa wakati.
Kwa ujumla, uzinduzi huu ni sehemu ya juhudi pana za Serikali ya Awamu ya Sita kuandaa nguvukazi ya Tanzania kwa ajili ya Dira ya 2050.
Kwa kutumia Akili Mnemba kutatua kero za mikopo, serikali inahakikisha kuwa vijana wanatumia muda mwingi kusoma na kufanya tafiti badala ya kupoteza muda mwingi wakifuatilia "bumu" au taarifa za mikopo. Huu ni ushahidi kuwa teknolojia ikitumika ipasavyo, inaweza kuwa daraja la uhakika la kuelekea maendeleo ya kweli.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464