Na Bora Mustafa - Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Joseph Mkude, amepongeza juhudi zinazofanywa na Umoja wa Waendesha Bodaboda Wilaya ya Arusha katika kuwawezesha vijana kupitia mpango wa ukopeshaji bodaboda.
Ametoa kauli hiyo leo wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliofanyika jijini Arusha, akisisitiza umuhimu wa nidhamu na uwajibikaji miongoni mwa waendesha bodaboda.
Aidha, Mhe. Mkude amesema kuwa serikali itaunga mkono juhudi hizo, ambapo ameahidi kugharamia vikundi kumi vya mwanzo vitakavyoundwa kwa ajili ya kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
“Ajali haina taarifa, hivyo ni muhimu waendesha bodaboda kuwa na bima ya afya itakayowasaidia wao na familia zao,” ameongeza.
Hata hivyo, ameeleza kuwepo kwa changamoto ya waendesha pikipiki wasiokuwa na usajili rasmi. Ametolea mfano wa ziara yake katika kituo cha polisi Murieth, ambapo alikuta pikipiki nyingi bila namba za usajili, akiweka wazi kuwa hali hiyo ni hatari na ni kinyume cha sheria.
Amefafanua kuwa kuna tofauti kubwa kati ya waendesha pikipiki na waendesha bodaboda, huku akisisitiza kuwa wanaovuruga amani kwa kiasi kikubwa ni waendesha pikipiki wasio rasmi.
Pia DC Mhe. Mkude amesisitiza umuhimu wa kuwa na utaratibu wa kutoa leseni kwa bei nafuu au kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwezesha vijana wengi zaidi kumiliki leseni na kuendesha shughuli zao kwa uhalali.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Wilaya ya Arusha, Richard Magembe, amesema kuwa mradi huo wa mikopo ya bodaboda ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha vijana kiuchumi.
Pia, ameainisha changamoto wanazokutana nazo ikiwemo ukosefu wa sare rasmi kwa waendesha bodaboda, jambo linaloathiri usalama wao na wa wananchi kwa ujumla.
Pamoja na hayo, ametoa wito kwa serikali na wadau wa maendeleo kushirikiana na bodaboda katika kuwawezesha zaidi kwa kuwapatia mafunzo na nyenzo muhimu za kazi.






