Wito huo ameutoa Ijumaa 09.01.2025 wakati akihitimisha Mkutano wa Tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Kamishna Mkuu Mwenda amesema kazi ya kukusanya kodi ni ya watumishi wote na siyo maafisa kodi pekee hivyo kila mtumishi wa TRA anapaswa kuhakikisha anatumia ubunifu, weledi na kuzingatia maadili ili kutimiza malengo ya TRA ya kukusanya Shilingi Trilioni 36.066 katika Mwaka wa Fedha 2025/26.
Aidha, amefafanua kuwa ni matumaini yake kuiona TRA inakusanya kodi kwa ufanisi na hatimaye kulifanya Taifa kujitegemea kupitia kodi zake.
"Na mimi ninatamani siku moja TRA iiwezeshe nchi yetu kuweza kujitegemea", amesema Kamishna Mkuu Mwenda.
Akizungumza kuhusu mikakati ya ukusanyaji kwa Nusu ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2025/26 Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA imejidhatiti kuhakikisha inaendelea kutumia mifumo katika ukusanyaji wa kodi huku akiutaja mfumo wa IDRAS ambao utaanza rasmi Febuari 9, 2026.
Mikakati mengine ni pamoja na kupambana na ukwepaji wa kodi, kuzuia magendo, kudhibiti mipaka, kuendelea kujenga uwezo wa watumishi katika taaluma zao ili waendelee kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha watumishi wa TRA wanakuwa na vifaa stahiki kutekeleza majukumu yao ili kuyatekeleza kwa ufanisi.
Mbali na hayo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia TRA watumishi wapya huku akitoa wito kwa viongozi kuwasimamia watumishi hao ili waweze kuleta tija katika utendaji wa majukumu yao.
Naye Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan mcha, amewataka watumishi wa TRA kuendelea kuboresha huduma kwa walipakodi, kutanua wigo wa walipakodi na kupambana na njia mbalimbali za ukwepaji wa kodi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Raslimali Watu na utawala TRA Bw. Moshi Jonathan Kabengwe amewapongeza wajumbe walioshiriki mkutano huo huku akiwataka kuzingatia yale yote waliyokubaliana katika Mkutano huo ili TRA iendelee kuvuka malengo ya Makusanyo.
Aidha, amewapongeza watumishi wa TRA wanaotarajiwa kustaafu ndani ya mwaka huu wa 2026 huku akisema kuwa watumishi hao wameacha alama katika utendaji wao wa kazi.
Mkutano huo wa Siku 5 wa kutathmini utendaji kazi wa TRA kwa Nusu ya Kwanza ya Mwaka wa fedha 2025/26 umeshirikisha jumla ya washiriki 477 kutoka katika ofisi za TRA nchi nzima.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464


