
Serikali imedhihirisha nia yake ya kuendelea kukuza uchumi wa ubunifu nchini (Creative Economy) baada ya Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, kutua eneo la Chanika, jijini Dar es Salaam, kukutana na kundi la watengeneza maudhui ya mtandao wa YouTube.
Kikao hicho kilichofanyika Jumamosi Januari 24, 2026, kilihusisha viongozi 40 wa vikundi vya utayarishaji ambavyo kwa pamoja vinasimamia zaidi ya wanatasnia 200 walioweka kambi katika viunga vya Chanika kwa ajili ya kuzalisha maudhui ya kidijitali.
Mapinduzi ya kiteknolojia yamegeuza simu na kamera kuwa ofisi kwa maelfu ya vijana nchini. Chanika sasa imekuwa kama "Hollywood" ndogo ya Dar es Salaam, ambapo ubunifu wa filamu fupi na mfululizo (Series) unawapatia vijana ajira na kuchangia kukuza mzunguko wa fedha na uchumi wa taifa.
Lengo kuu la ujio wa Dkt. Kasiga lilikuwa ni kusikiliza mapigo ya moyo ya wanatasnia hao, kubaini changamoto zinazowakabili, na kutoa elimu ya umuhimu wa kujirasimisha kisheria ili kutambulika na serikali na kufurahia fursa pana zaidi.
Katika kikao hicho, watengeneza maudhui hao walimwaga hoja mbalimbali ambazo zimekuwa zikikwamisha kasi ya ukuaji wa soko la filamu za YouTube. Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na uhitaji wa mafunzo ya kitaalamu katika ufundi wa kamera, uandishi wa miswada na uhariri wa picha.
Aidha, walitaja changamoto ya uwezeshwaji wa kifedha ili kuboresha vifaa vya utayarishaji pamoja na hitaji la marekebisho ya sheria ya filamu ili iendane na kasi ya maendeleo ya kidijitali. Vilevile, walishauri uanzishwaji wa mifumo mipya ya usambazaji ili filamu hizo ziweze kuleta tija zaidi ndani na nje ya nchi.
Dkt. Kasiga amewapongeza wanatasnia wa Chanika kwa uthubutu wao wa kuwekeza muda, fedha, na akili katika kuzalisha kazi zinazoburudisha na kuelimisha jamii.
Amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango wao na iko tayari kuwabeba.
Alisisitiza kuwa Bodi ya Filamu ipo kwa ajili ya kuwahudumia na ameahidi kuitisha vikao na taasisi nyingine wadau ili kuhakikisha wanapata majibu ya moja kwa moja kuhusu changamoto zao. Pia, amewahimiza vijana hao kutumia mazingira wezeshi yaliyowekwa na Rais Samia kwa kujirasimisha rasmi, akieleza kuwa kujisajili siyo tu kutekeleza sheria, bali ni ufunguo wa kupata mikopo, ruzuku, na ulinzi wa kazi zao.
Ujio huo wa Bodi ya Filamu huko Chanika ni alama kuwa serikali sasa inahamishia nguvu zake kule ambako vijana wapo, yaani kwenye mitandao ya kijamii. Ni matarajio ya wengi kuwa kurasimishwa kwa majeshi haya ya YouTube kutaifanya tasnia ya filamu Tanzania kuwa na ushindani mkubwa katika soko la kimataifa na kuongeza pato la taifa kupitia sanaa.
Kwa kuanza na kambi za Chanika, serikali inaweka msingi wa kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha maudhui ya kidijitali barani Afrika.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464