` RC MHITA: WAFANYABIASHARA WALIOPISHA UJENZI WA SOKO LA MAGANZO WAPEWE KIPAUMBELE

RC MHITA: WAFANYABIASHARA WALIOPISHA UJENZI WA SOKO LA MAGANZO WAPEWE KIPAUMBELE

Na Johnson James, KISHAPU

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ametoa agizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika soko la zamani la Maganzo wanapewa kipaumbele cha kurejea katika soko hilo jipya mara baada ya kukamilika kwa ujenzi.

Mhe. Mhita alitoa agizo hilo Januari 10, 2026, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko hilo la kisasa linalojengwa kwa ufadhili wa Kampuni ya Mwadui kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR).

“Ni muhimu wafanyabiashara waliopisha ujenzi huu wapewe nafasi za kwanza. Hawa ndio walikuwa kwenye soko hili, wakilipa ushuru na kuchangia mapato ya Halmashauri. Si vyema wakaachwa,” alisisitiza RC Mhita.

Akitoa kilio chao mbele ya Mkuu wa Mkoa, mfanyabiashara Simon Andrea aliiomba Serikali kuhakikisha soko hilo linakamilika na kuanza kutumika haraka ili kuwanusuru dhidi ya hasara wanayoipata kutokana na mazingira duni ya sasa ya kufanyia biashara.

“Biashara zetu zinaharibika, hatuna eneo rafiki. Tunaomba Mhe. RC usimamie hili soko likamilike na tuanze kulitumia,” alisema Andrea.

Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Bi. Hilda Hozza kutoka mgodi wa Mwadui, alisema soko hilo linajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 260 na litakuwa na vizimba 200. Aliongeza kuwa hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Soko hilo la Maganzo linatarajiwa kuwa mkombozi kwa wafanyabiashara zaidi ya 200, likiwa na miundombinu rafiki na ya kisasa, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Kishapu na Mkoa kwa ujumla.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464