` VIJANA JIULIZENI WACHOCHEZI KWANINI WANANG'ANG'ANI TANZANIA NA SIO UGANDA

VIJANA JIULIZENI WACHOCHEZI KWANINI WANANG'ANG'ANI TANZANIA NA SIO UGANDA


Katika mwendelezo wa mijadala inayoendelea nchini kuhusu amani na usalama, Watanzania wamehimizwa kuamka na kutambua malengo halisi ya wanaochochea vurugu na machafuko, huku wito ukitolewa kwa vijana kutotumiwa bila kujua.

Ujumbe huo, uliochapishwa na Alphanga Black umesisitiza kuwa vurugu nchini Tanzania huchochewa kwa lengo la kudhoofisha mamlaka ya taifa na kufanya iwe rahisi kwa nguvu za nje kuingia kama "wasuluhishi" au "watoa misaada," huku wakisukuma masharti yanayodhoofisha mamlaka ya taifa letu.

Maslahi ya Madini 

Mtoa ujumbe ameeleza kuwa malengo ya wanaochochea vurugu nchini hayafanani kabisa na matarajio ya vijana wanaotumiwa, akiongeza kuwa vijana wa Tanzania wanatambua thamani ya umoja na amani katika kulinda rasilimali za nchi dhidi ya wanyonyaji.

Alihoji ni kwanini kelele na uchochezi vinaelekezwa zaidi Tanzania hasa baada ya taifa kuanza kusimamia rasilimali zake kwa umakini, huku akitaja ugunduzi wa madini ya Uranium kama moja ya sababu zinazoweza kulifanya Taifa kulengwa na propaganda.

"Rasilimali zetu, ikiwemo Uranium, ni mali ya Watanzania wote—si fursa ya wageni wanaotaka kuitumia kupitia milango ya machafuko," alisisitiza.

Uganda Kama Mfano wa Ukimya

Katika kuonyesha tofauti ya uelekeo wa vyombo vya habari vya kimataifa, ujumbe huo ulisisitiza umuhimu wa kufuatilia kinachoendelea nchini Uganda, ambako kumekuwa na ukimya kutoka kwa vyombo vikubwa vya habari duniani na wanaharakati wa kigeni hasa wale waliopo Kenya.

Uchunguzi huo uliibua maswali:kama Je, kuna viongozi wa dini kule (Uganda) wanaotoa kauli kali?Je, kuna vyombo vikubwa vya habari duniani vikitoa mijadala mizito kuhusu Uganda?Je, kuna wanaharakati wa Kenya, Ulaya, au mashirika ya nje yanayopaza sauti kama wanavyofanya kuhusu Tanzania?

Akijibu maswali hayo, mtoa ujumbe alisema kuna "Kimya. Hakuna kelele," akihimiza vijana wajue vita hii ni ya nini na wanaotumwa wanapata nini.

Wito wa Uzalendo na Ufahamu

Kama hitimisho, Watanzania wamehimizwa kuamka na kutambua kuwa amani ya Tanzania si udhaifu, bali ni nguvu, na umoja wake ni urithi.

Ujumbe huo ulimalizika kwa kutoa wito kwa vijana kupewa elimu na ufahamu wa kujua propaganda ya dunia inataka nini, huku akiwaomba Watanzania wote waunge mkono viongozi katika kutetea Taifa, ili machafuko yasifikishe nchi mahali pabaya pa kudidimizwa uwezo wa viongozi. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464